Nenda kwa yaliyomo

Pandemia

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Mazishi ya wahanga wa pandemia ya tauni wakati wa karne ya 13 huko Ufaransa (mchoro katika muswada "The Chronicles of Gilles Li Muisis" (1272-1352), Bibliothèque royale de Belgique, MS 13076-77, f. 24v.

Pandemia (kutoka Kigiriki παν pan -ote + δήμος demos watu) inamaanisha uenezi wa ugonjwa wa kuambukiza katika eneo kubwa, kwa mfano bara au hata duniani kote.

Kwa kawaida uenezi wa ugonjwa huitwa "epidemia": neno hili lamaanisha kuongezeka kwa wagonjwa kwenye eneo au kikundi, tena katika kipindi fulani. Kama epidemia inapanuka kimataifa inafikia ngazi ya "pandemia".

Mifano ya pandemia za kihistoria

[hariri | hariri chanzo]

Historia imehifadhi habari za pandemia mbalimbali. Kwa habari za kale sana si rahisi kuwa na uhakika ulikuwa ugonjwa gani uliosababisha vifo vilivyotajwa.

Lakini tangu zama za kati kuna habari za pandemia za tauni zilizoua milioni kadhaa za watu. Hasa pandemia ya tauni ya karne ya 14 inajulikana iliua watu milioni 25 yaani theluthi moja ya wakazi wa Ulaya wa siku zile.

Katika karne ya 20 ilikuwa hasa pandemia ya homa ya mafua iliyoitwa "influenza ya Kihispania" ambayo iliambukiza watu milioni 500 na kuua milioni 20-25 kote duniani kati ya miaka 1918 na 1920. Inakadiriwa ya kwamba kati yao laki kadhaa walikufa Afrika ya Mashariki.

Tangu mwaka 1980 pandemia ya UKIMWI imeendelea kuenea kote duniani na kuua takriban watu milioni 37 hadi sasa.

Tofauti kati ya pandemia na magonjwa mengine yanayoua

[hariri | hariri chanzo]

Shirika la Afya Duniani (WHO) imeeleza pandemia kuwa na vigezo 3:

  • kutokea kwa ugonjwa ambao ni mgeni katika jamii inayoathiriwa
  • ni wanadamu wanaoambukizwa na kuwa wagonjwa sana
  • virusi au bakteria zinazosababisha ugonjwa zinaenea kwa urahisi kati ya watu

Si kila ugonjwa unaoua watu wengi unaweza kuitwa pandemia: lazima uwe ugonjwa wa kuambukizwa. Kwa mfano kansa inaua watu wengi lakini si pandemia kwa sababu kansa si ugonjwa wa kuambukiza.

Si kila ugonjwa mkali unaweza kuendelea kuwa pandemia. Maana kama ugonjwa ni mkali mno unaua wahanga wake haraka na hivyo kuzuia uenezi wake. Mfano mmojawapo ni homa ya Ebola ambayo ni kati ya magonjwa hatari zaidi, lakini haikuendelea kupitia ngazi ya epidemia.

Uenezi wa pandemia

[hariri | hariri chanzo]

Leo hii pandemia zinaenea hasa kwa kufuata njia za mawasiliano kwa eropleni. UKIMWI iliyokuwa tatizo la kieneo likaenea kwa njia ya utalii wa kimataifa kuwa ugonjwa unaopatikana kote duniani.

Wakati wa pandemia ya SARS mwaka 2002/2003 ilionekana ya kwamba katika Asia, yenye asili ya maambukizo ugonjwa ulienea kwa kasi ya wastani, ila huko Kanada idadi ilianza kuongezeka haraka - kutokana na kufika kwa watalii na wafanyabiashara waliorudi kwao kutoka Asia kwa ndege.

Tauni ilifika Ulaya kwa njia ya meli za biashara kutoka Asia.

Magonjwa yalienea hata zamani pasipo usafiri wa kisasa lakini uenezi ulikuwa wa polepole zaidi na mara nyingi jiografia ilizuia kufika kwa magonjwa fulani kwenye visiwa au ng'ambo ya milima mirefu.

Ngazi za pandemia ya homa ya mafua kufuatana na WHO

[hariri | hariri chanzo]

Shirika la Afya Duniani (WHO) imetunga mpango wa kujiandaa kwa kutokea kwa virusi mpya za homa ya mafua. Hapo imeeleza ngazi 6 za uenezi wa pandemia pamoja na mapendekezo kuhusu hatua zinazopaswa kuchukuliwa na serikali za nchi husika.

Kipindi kabla ya pandemia:

  • ngazi 1: hakuna aina mpya ya virusi ya homa ya mafua inayotazamiwa kwa binadamu
  • ngazi 2: aina mpya ya virusi ya homa ya mafua imefunduliwa kwa wanyama, haikupita bado kwa wanadamu

Kipindi cha tahadhari ya pandemia:

  • ngazi 3: watu wameanza kuambukizwa na aina hiyo mpya ya virusi kwa njia ya wanyama, lakini maambukizo hayakuenea bado kutoka mtu kwa mtu
  • ngazi 4: kuna vikundi vidogo vya wagonjwa, lakini uenezi wa virusi kutoka mtu kwenda mtu mwingine bado inaendelea polepole
  • ngazi 5: vikundi vya wagonjwa vinaongezeka, lakini uenezi bado umebaki katika maeneo fulani

Kipindi cha Pandemia:

  • ngazi 6: Pandemia: uambukizaji unazidi kuenea katika jamii kwa jumla

Tazama pia

[hariri | hariri chanzo]
  • Steward's "The Next Global Threat: Pandemic Influenza".

Viungo vya nje

[hariri | hariri chanzo]
Makala hii kuhusu mambo ya tiba bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Pandemia kama sababu yake au mahusiano yake na mada nyingine?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.