Majuro
Majuro ni atolli yenye nafasi ya mji mkuu wa nchi ya Visiwa vya Marshall mwenye wakazi 25,400. Atolli yote ina visiwa vidogo 64 lakini hasa kanda mbili ndefu na nyembamba zinazounganishwa kwa daraja karibu na uwanja wa ndege. Eneo lote la nchi kavu ni 9.7 km². Mviringo wa visiwa vyake umezungusha hori la ndani lenye eneo la 295 km² za maji.
Wakazi walio wengi hukaa kwenye kisiwa kirefu cha mashariki katika miji ya Delap, Uliga na Darrit (au: Djarot). Hii mitatu huitwa mara nyingi kwa kifupi D-U-D ikionekana kama mji moja.
Uliga ni sehemu cha biashara penye maduka, benki na chuo cha Marshall. Ofisi za serikali ziko hasa Delap kuna pia maduka. Darrit ina hasa nyumba za watu pamoja na shule. Kwenye mwisho wa kisiwa kirefu kaskazini ya Darrit kuna mtaa wa vibanda unaoitwa Rita.
Wakimbizi kutoka Bikini wanakaa hasa kwenye kisiwa kidogo cha Ejit kando la Rita.
Upande wa magharibi wa kisiwa kirefu huitwa "Laura" ni eneo lenye rutba na mashamba. Watu wenye pesa wameanza kujenga nyumba hapa pia.