Nenda kwa yaliyomo

Nyota nova

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Pitio kulingana na tarehe 17:14, 26 Februari 2018 na Kipala (majadiliano | michango)

Nyota nova (lat. stella nova kwa maana ya "nyota mpya", ing. nova) ni ongezeko la ghafla la mwangaza wa nyota. Ilhali idadi kubwa za nyota hazionekani kwa macho matupu ongezeko hili linatokea mara nyingi kama "nyota mpya" angani inayoweza kung'aa sana hata kushinda nyota zote nyingine. Hivyo inaonekana kwa muda tu ikipotea baadaye tena kwa mtazamaji asiye na darubini.

Historia ya utazamaji

Zamani nyota zote zilizowaka hivi ziliitwa kwa jina lilelile "nova". Jina hili lilitumiwa mara ya kwanza na Tycho Brahe aliyeona kwenye mwaka 1572 nyota mpya katika eneo la kundinyota Mke wa Kurusi (Cassiopeia) na kueleza utafiti wake katika kitabu cha "De stella nova" [1]. Tycho Brahe alianzisha wakati ule amjadiliano kuhusu mafundisho ya wataalamu wa kale walioamini ya kwamba hakuna mabadiliko kwenye anga ya nyota.

Lakini kuna taarifa za kale kuhusu nyota mpya zilizotokea angani na ile ya kale zaidi ni ya wanaastronomia Wachina wa mwaka 185 kuhu nyota geni iliyoonekana karibu na Rijili Kantori (α Centauri). Nova nyingine ilitazamiwa mwaka 1006 na kurekodiwa na wanaastronomia Wachina, Wajapani na Wakristo wa Baghdad, mabaki yake huonekana hadi leo kama "Nebula ya Kaa" katika eneo la Tauri (Taurus).

Tofauti kati ya Nova na Supanova

Tangu katikati ya karne ya 20 vipimo vilileta wanaastronomia kutofautisha kati ya "nova" na "supanova" ambazo zote ni "nyota mpya" zinazotokea angani kwa muda lakini kwa sababu tofauti.

  • Nova ya Tycho Brahe sawa na ile ya mwaka 1006 siku hizi zinaitwa "supanova" maana zilikuwa milipuko ya nyota zilizoharibika kutokana na matukio haya. Inayobaki ni wingu la mata yake iliyosambaa katika eneo kubwa kama Nebula ya Kaa.
  • Neno "nova" linataja sasa kuwaka kwa muda kwa nyota ndani ya mfumo wa nyota pacha. Katika hali ya nova nyota inaongeza mwangaza ghafla mara elfu kadhaa ya kawaida yake hadi kurudi tena baada ya wiki au miezi katika hali yake kama kabla ya kuwaka.


Tabia za nova

Nyota Kibete Cheupe inavuta mata kutoka Jitu Jekundu jirani kwake.

Nyota nova za kawaida zinatokea katika mfumo wa nyota pacha. Nadharia inayokubalika na wengi inasema: nyota kibete cheupe na nyota kubwa, hasa jitu jekundu, zinazungukana kwa umbali wa karibu. Kibete cheupe kimeshamaliza hidrojeni yake na kujikaza, hivyo graviti yake bado ni kubwa ingawa mjao wake ni mdogo, pia ni joto sana. Jitu jekundu la jirani linaendelea kupanuka. Hapa sehemu ya mata ya tabaka za nje ya nyota kubwa inavutwa na graviti ya nyota ndogo na kuhamia upande wake. Sehemu ya mata hii ni hidrojeni inayokusanyika kwa umbo la diski ya uongezekaji[2] inayozunguka Kibete Cheupe na hatimaye kushuka chini zaidi kama angahewa. Hidrojeni hii inapashwa moto na uso wa Kibete Cheupe hadi kufikia halijoto ya kutosha ya kuanzisha myeyungano wa kinyuklia (nuclear fusion).

Mchakato huu unaachisha kiasi kikubwa cha nishati inayorusha sehemu ya hidrojeni inayowaka kwenye anga la nje. Hii inaongeza mwangaza wa nyota inayoonekana sasa kama nyota nova. Kiasi cha masi inayorushwa angani wakati wa kuwaka inakadiriwa kuwa takriban M 1/10,000.

Maendeleo ya nova inafuata hatua kama hizi:

  • wakati myeyungano wa kinyuklia unaanza usoni mwa Kibete Cheupe mwangaza wake unaongezeka takriban mag 9 katika kipindi cha siku chache.
  • mara nyingi mwangaza unabaki palepale kwa siku kadhaa; hatua hii haikutazamiwa kwa kila nova
  • baada ya siku hadi wiki kadhaa mwangaza unaongezeka tena mnamo mag 2.
  • kutoka kilele hiki mwangaza unaanza kupungua mnamo mag 3.5
  • katika hatua inayofuata kuna kupoa tena, manmo mag 3, atika muda wa miezi hadi miaka kadhaa
  • katika miaka au miongo inayofuata mwangaza unaendelea kupungua hadi kufikia tena hali ya awali.

Nova za kurudia

Kinadharia mchakato huu unaweza kurudia mara kadhaa kwa sababu baada ya mlipuko wa angahewa ya nyota ndogo mata kutoka jirani mkubwa inaanza kuvutwa tena. Nyota RS Ophiuchi katika kundinyota ya Hawaa ilitazamiwa kuwaka mara sita[3]: 1898, 1933, 1958, 1967, 1985 na 2006. Hadi sasa kuna nyota nova 10 zilizotazamiwa kuwaka tena kati ya takriban 400 zilizogunduliwa katika Njia Nyeupe[4]; kwa hiyo hakuna uhakika bado kuhusu muda wa kawaida uliopo baina ya kuwaka kwa nyota. Kama nyota kibete imeendelea kukusanya mata nyingi kuna uwezekano ya kwamba mwishoni inalipuka kama supanova [5]

Kila mwaka kuna takriban nyota nova 10 zinazotazamiwa katika Njia Nyeupe[6]. Lakini wanaastronomia hukadiria ya kwamba idadi halisi ni kubwa zaidi, labda mnamo 50 kila mwaka katika galaksi yetu[7].

Nyota nova zinagunduliwa pia katika galaksi nyingine, kwa mfano katika galaksi ya Andromeda (M31) na penginepo[8].

Tanbihi

  1. Kilatini kwa "Kuhusu nyota mpya", linganisha Tycho's Supernova Remnant, tovuti ya NASA, iliangaliwa Februari 2108
  2. ing. "accretion disk"
  3. Brandi, E.; Quiroga, C.; Mikołajewska, J. (2009). "Spectroscopic orbits and variations of RS Ophiuchi". Astronomy and Astrophysics. 497
  4. M. J. Darnley, V. A. R. M. Ribeiro1,2, M. F. Bode, R. A. Hounsell, and R. P. Williams, ON THE PROGENITORS OF GALACTIC NOVAE, The Astrophysical Journal, Volume 746, Number 1, Published 2012 January 25
  5. Sababu yake ni ya kwamba graviti yake inaweza kuzidi shinikizo ya mnururisho ndani yake ambayo kwa kawaida inatunza uwiano ndani ya nyota
  6. List of Novae in the Milky Way, tovuti ya Central Bureau for Astronomical Telegrams, iliangaliwa Februari 2018
  7. Shafter, A.W. (January 2017). "The Galactic Nova Rate Revisited". The Astrophysical Journal. 834 (2): 192–203
  8. M31 (Apparent) Novae Page, tovuti ya Central Bureau for Astronomical Telegrams, iliangaliwa Februari 2018