Mawaziri wa Fedha wa G20 kujadili kuwatoza kodi mabilionea
26 Julai 2024Ajenda hiyo ndio kipaumbele cha juu cha Brazil ambayo sasa inashikilia urais wa kupokeza wa kundi la G20.
Mkutano huo wa mjini Rio de Janeiro unatazamiwa kuwa muhimu kwa sababu kwa mara ya kwanza nchi zenye usemi duniani zinajadili pendekezo la kuwatoza kodi watu wenye utajiri uliopindukia.
Pendekezo lililo mezani linataka kuwepo sera ya kimataifa ya kuwatoza kodi ya mapato ya asilimia mbili watu wote wenye ukwasi unaozidi dola bilioni moja za Marekani.
Waziri wa Fedha wa Brazil ambaye ndiye mwenyeji wa mkutano wa Rio, Fernando Haddad amewaambia waandishi habari kwamba azimio la mwisho la mkutano huo wa siku mbili litajumuisha pendekezo hilo la kuwatoza kodi matajiri lakini hakufafanua iwapo kiwango cha asilimia 2 kinachoshinikizwa na nchi yake kitawekwa kwa maandishi.
Pendekezo la Brazil yazusha mgawanyiko miongoni mwa nchi za G20
Hata hivyo tayari pendekezo hilo la Brazil limezusha mgawanyiko miongoni mwa nchi wanachama wa kundi la G20. Marekani imelipinga mara moja wazo hilo ikisema hakuna haja ya kuwepo sera ya ulimwengu inayoweka kiwango cha kodi kinachopaswa kutozwa wale wenye utajiri wa kupindukia.
Hata kabla ya kuanza mkutano wa hii leo, Waziri wa Fedha wa Marekani Janet Yellen amelipinga pendekezo la Brazil akisema itakuwa vigumu kutekeleza sera ya kuwatoza kodi mabilionea katika ngazi ya kimataifa. Badala yake Yellen amesema Washington inaamini kila nchi inaweza kutengeneza mfumo wake wa kikodi wa kukusanya mapato kutoka kwa mabilionea.
Miito ya kuundwa sera ya kimataifa ya kuwatoza kodi ya mapato mabilionea imeongezeka miaka ya karibuni lakini tofauti za mtazamo miongoni mwa mataifa yenye nguvu kiuchumi yamefanya iwe vigumu pendekezo kama hilo kuafikiwa.
Hata hivyo Rais Inacio Lula da Silva wa Brazil ambaye anapendelea sera za uchumi zinazowapiga jeki watu masikini amesema nchi yake imejipa jukumu la kupigia debe suala hilo na kutafuta uungaji mkono wa kimataifa.
Kwenye mkutano wa mjini Rio, pendekezo hilo la Brazil linaungwa mkono na Ufaransa, Uhispania, Afrika Kusini pamoja na Umoja wa Afrika ambao ulipata kiti ndani ya kundi la G20 mwaka uliopita.
Pengo la kipato ndio chimbuko la madai ya kodi kwa mabilionea
Tofauti ya kipato imezidi kutanuka kote duniani katika miaka ya karibuni. Tathmini hiyo ni kulingana na shirika la kimataifa la masuala ya ustawi na maendeleo Oxfam.
Utafiti wao wa hivi karibuni unaonesha asilimia moja ya watu wote duniani wanamiliki utajiri usio na mfano ambao kundi hilo dogo la watu mabilionea lilijiingizia zaidi ya dola trilioni 40 katika kipindi cha miaka 10 iliyopita.
Lakini licha ya ukwasi wote huo kundi hilo la matajiri limelipa kiwango kidogo cha kodi kwa sababu hivi sasa kwa wastani mabilionia wanatozwa asilimia 0.3 pekee ya mapato yao.
Pendekezo la Brazil la kupandisha kiwango hicho hadi asilimia 2 inatazamiwa kukusanya dola bilioni 200 hadi 250 kwa mwaka kutoka kundi la mabilioni 3,000 walio na utajiri wa zaidi ya dola bilioni 1.
Nchi zinazopigia upatu sera hiyo zinasema kiwango hicho cha fedha kitakachokusanywa kitasaidia utoaji huduma za jamii kama afya na elimu pamoja na mapambano dhidi ya athari za mabadiliko ya tabinchi.