Nenda kwa yaliyomo

Mhindi (kundinyota)

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru

Kwa maana tofauti ya jina hili tazama Muhindi na Uhindi

Nyota za kundinyota Mhindi (Indus) katika sehemu yao ya angani

Mhindi (kwa Kilatini na Kiingereza Indus) [1] ni jina la kundinyota linaloonekana katika angakusi ya Dunia yetu.

Mahali pake

Mhindi linapatikana kati ya nyota angavu za Alnair (α Alfa Gruis) katika Kuruki na Peacock (α Alfa Pavi) katika Tausi. Linapakana na makundinyota ya Kuruki (Grus) na Hadubini ( Microscopium) upande wa kaskazini, Darubini (en: Telescopium) na Tausi (Pavo) upande wa mashariki, Thumni (Octans) upande wa kusini na Tukani (Tucana) upande wa magharibi.

Jina

Mhindi linapatikana kati ya makundinyota yaliyobuniwa tangu mabaharia Wazungu kuzunguka dunia yote katika karne ya 16 na kuona mara ya kwanza nyota za kusini. Nyingi hazikutajwa katika vitabu vya Wagiriki wa Kale au Waarabu. Kundinyota hili lilibuniwa mara ya kwanza na mabaharia Waholanzi Pieter Dirkszoon Keyser na Frederick de Houtman katika safari yao ya kuelekea Indonesia likaonyeshwa mara ya kwanza mwaka 1598 katika globu ya nyota ya Petrus Plancius na kupokelewa katika “Uranometria” ya Johann Bayer.

Keyser alitumia jina la Kiholanzi “De Indiaen” (yaani Mhindi) lililotajwa baadaye kwa jina la Kilatini „Indus“. Jina hili alilitumia kama kumbukumbu ya watu aliowaona mara ya kwanza katika maisha yake kwenye eneo la Bahari ya Hindi pale Madagaska na kwenye visiwa vya Indonesia. Baadaye alichukuliwa mara kadhaa kwa maana ya “Wahindi Wekundu” yaani Maindio wa Marekani ambayo si maana ya kiasili.

Leo Mhindi lipo pia katika orodha ya makundinyota 88 yanayoorodheshwa na Umoja wa Kimataifa wa Astronomia [2]. Kifupi chake rasmi kufuatana na Ukia ni 'Ind'.[3]

Nyota

Mhindi haina nayota angavu sana. Nyota angavu zaidi ni α Alfa Indi yenye mwangaza unaoonekana wa mag 3.1 ikiwa umbali kutoka Dunia wa miakanuru 101[4]. Beta Indi ina mag 3.7 ipo kwa umbali wa miakanuru 600 kutoka kwetu. Delta Indi ina mag 4.4 na ipo umbali wa miakanuru 185.

Epsilon Indi yenye mag 4.69 ni kati ya nyota zilizo karibu sana na Dunia ikiwa na umbali wa miakanuru 11.8.

Tanbihi

  1. Uhusika milikishi (en:genitive) ya neno "Indus" katika lugha ya Kilatini ni "Indi" na hili ni umbo la jina linaloonekana katika majina ya nyota za kundi hili kama vile Alfa Indi, nk.
  2. The Constellations, tovuti ya International Astronomical Union , iliangaliwa Julai 2017
  3. Russell, Henry Norris (1922). "The New International Symbols for the Constellations". Popular Astronomy. 30: 469–71. Bibcode:1922PA.....30..469R.
  4. [ http://stars.astro.illinois.edu/sow/persian.html The Persian (Alpha Indi)], tovuti ya Prof. Jim Kaler, university of Illinois, iliangaliwa Oktoba 2017; Kaler anatumia kwa nyota hii jina la Kichina “The Persian” isiyo kawaida

Viungo vya Nje