Nenda kwa yaliyomo

Mawasiliano

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Alama ya mawasiliano ya simu

Mawasiliano kwa kawaida hufafanuliwa kama kupashana au kubadilishana mawazo, maoni, hisia au habari kwa maneno, maandishi au ishara kufikia lengo lililokubaliwa au mwelekeo uliokubaliwa (habari)[1].

Ingawa kuna mawasiliano ya njia moja, mawasiliano yanaweza kueleweka vyema kama mchakato wa kuhamisha taarifa kati ya wahusika wawili.

Katika mawasiliano habari hupakiwa na kutumwa na kupashwa na mtu kwa anayepokea kupitia njia maalum. Kisha anayepokea hupakua ujumbe ule na kumpatia aliyetuma (ma)jibu. Aina zote za mawasiliano huhitaji mtumaji, ujumbe na mpokeaji.

Mawasiliano huhitaji kwamba wanaohusika wawe na jambo linalowaunganisha. Kuna njia zinazohusisha kusikia, kama vile unenaji, wimbo, na toni ya sauti, na kuna zile zisizohusisha kusikia, kama vile miondoko ya mwili, lugha ishara, kugusa, kuwasiliana kwa macho na kuandika.

Mabadiliko katika mawasiliano

[hariri | hariri chanzo]

Kadiri wakati unavyopita, teknolojia imeendelea kukua na kuibua aina mpya za mawazo kuhusu mawasiliano. Maendeleo hayo ya teknolojia yalibadilisha jinsi mawasiliano yanavyofanyika. Watafiti wamegawanya jinsi mawasiliano yalivyobadilika katika hatua tatu.

Mabadiliko ya mwanzo: mawasiliano ya kwanza katika maandishi yalianza na michoro. Maandishi hayo yaliandikwa kwenye mawe, ambayo yalikuwa mazito mno kuhamishwa. Wakati huo, mawasiliano ya maandishi hayangeweza kubebwa, ingawa yalikuwepo.

Mabadiliko ya pili: maandishi yalianza kufanyiwa kwenye karatasi, mavunjo, udongo, nta, n.k. Herufi za alfabeti zilibuniwa, hivyo basi kuruhusu mfanano wa lugha katika maeneo makubwa. Baada ya muda, shirika la uchapishaji la Gutenberg lilianzishwa. Gutenberg alitayarisha kitabu cha kwanza cha kuchapishwa akitumia mashine yake, na kitabu hicho kilikuwa Biblia. Maandiko hayo yaliweza kusafirishwa kwa watu wengine duniani ili wayaone, pia yaliweza kuhifadhiwa na kubebwa.

Mabadiliko ya tatu: taarifa sasa inaweza kuhamishwa kupitia mawimbi, na ishara za kielektroniki.

Kwa hiyo mawasiliano ni njia inayotumiwa katika kutoa na kufikisha maana katika jaribio la kusababisha ufahamu wa jumla. Utaratibu huu unahitaji mkusanyiko mkubwa wa ujuzi wa mawasiliano miongoni mwa na baina ya watu, kusikiliza, kutazama, kuongea, kuhoji, kuchambua na kutathmini. Ni kupitia mawasiliano kwamba ushirikiano hutokea. [2]

Pia kuna vikwazo vingi vya kawaida katika mawasiliano. Viwili kati yake vikiwa kupasha ujumbe kupita kiasi (mtu anapopokea ujumbe mwingi mno kwa wakati mmoja), na ujumbe changamano.

Aina za mawasiliano

[hariri | hariri chanzo]

Kuna sehemu tatu kuu katika mawasiliano ya ana kwa ana kati ya binadamu: miondoko ya mwili, toni ya sauti na maneno.

Kulingana na utafiti: [3]

  • 55% ya athari hulingana na miondoko ya mwili. Kwa mfano: jinsi mtu alivyokaa, ishara za uso, mikono na macho
  • 38% hulingana na toni ya sauti, na
  • 7% hulingana na maudhui (ujumbe au maneno) yaliyotumika katika mchakato wa mawasiliano.

Ingawa asilimia ya ushawishi inaweza ikabadilika kwa sababu tofauti, kama vile msikilizaji na msemaji, mawasiliano kwa jumla hulenga kutimiza lengo moja, kwa hiyo, katika baadhi ya matukio, huwa yanafanana kote duniani. Mfumo wa ishara, kama vile sauti, kiimbo au uzito wa sauti, ishara za mikono au za uso au ishara zilizoandikwa ambazo huwasilisha mawazo au hisia.

Ikiwa lugha inahusu kuwasiliana kwa ishara, sauti, mlio, ishara za uso na za mikono, au ishara zilizoandikwa, je, mawasiliano ya wanyama yanaweza kuchukuliwa kama lugha? Wanyama hawana lugha iliyoandikwa, lakini baadhi wanadhani mawasiliano ya wanyama yanaweza kuchukuliwa kama lugha ya namna yake.

Lugha za binadamu zinazozungumzwa na kuandikwa zinaweza kufafanuliwa kama mfumo wa ishara (zinazojulikana wakati mwingine kama leksia na sarufi) ambayo ishara hizo huzingatia. Neno "lugha" pia hutumika kurejelea sifa bainifu za lugha.

Kujifunza lugha ni jambo la kawaida katika utoto wa binadamu. Lugha nyingi hutumia mifumo ya sauti au ishara ambazo huwezesha mawasiliano baina ya mtu na wenzake. Kuna maelfu ya lugha, nazo huwa na sifa bainifu, ingawa nyingi ya sifa hizi huwa na upekee.

Hakuna mgawanyo dhahiri kati ya lugha na lahaja, lakini mwanaisimu Weinreich Max anatambuliwa kwa kusema kuwa "lugha ni lahaja iliyo na jeshi la nchi kavu na la majini". Lugha za kuundwa kama vile Kiesperanto, lugha za tarakilishi, na maumbo mbalimbali ya hisabati haziko chini ya sifa bainifu zinazohusisha lugha za binadamu.

Mawasiliano kwa ishara/kutazama

[hariri | hariri chanzo]

Mawasiliano kwa ishara ni mchakato wa kuwasiliana kwa njia ya kutuma na kupokea ujumbe usiohusisha maneno. Ujumbe kama huo unaweza kuwasilishwa kupitia ishara za uso au mikono, miondoko ya mwili au jinsi ya kukaa; ishara ya uso na kutazamana machoni, mawasiliano kwa njia ya vitu, kama vile mavazi uliyovalia, jinsi ulivyotengeza nywele, au hata kwa michoro, pia kupitia jumla ya njia zilizoandikwa hapo juu, kama vile mawasiliano kupitia tabia. Mawasiliano kwa ishara huwa na jukumu muhimu katika maisha ya kila siku ya kila mtu, iwe ni katika uhusiano wa kiajira hadi wa kimapenzi.

Mazungumzo pia huwa na vipengele vya mawasiliano kwa ishara yanayojulikana kama 'viziada-lugha' ('paralanguage'), ambayo huhusisha ubora wa sauti, hisia na mitindo ya kuzungumza, ikiwa pamoja na sifa za kiarudhi kama vile mdundo, lafudhi na msisitizo.

Aidha, matini zilizoandikwa zina vipengele vya mawasiliano kwa ishara kama vile mtindo wa kuandika, mpangilio wa maneno, au matumizi ya hisia. Neno lililounganisha maneno ya Kiingereza ya hisia (emote) na ikoni (icon), kihisishi (emoticon) ni ishara au muungano wa ishara zinazotumiwa kupitisha hisia katika maandishi.

Aina nyingine za mawasiliano kama vile telegrafia huwa katika kategoria hii, ambapo ishara hupitishwa kutoka kwa mtu mmoja hadi mwingine kwa njia tofauti. Ishara hizo zinaweza kuwa viwakilishi vya maneno, vifaa au makadirio tu. Majaribio yameonyesha kwamba binadamu wanaweza kuwasiliana moja kwa moja kupitia njia hii [4] bila miondoko ya kimwili, toni ya sauti au maneno.

Kategoria na sifa GW Porter anagawanya mawasiliano kwa ishara katika kategoria nne:

  1. Kimwili. Hii ni aina ya mawasiliano ya binafsi. Mawasiliano hayo yanahusisha ishara za uso, toni ya sauti, kugusa, kunusa, na miondoko ya mwili.
  2. Ujumi. Hii ni aina ya mawasiliano ambayo hufanyika kupitia njia za ubunifu: kucheza ala ya muziki, dansi, uchoraji na uchongaji.
  3. Ishara. Hii ni aina ya mawasiliano, ambayo inajumuisha matumizi ya bendera za ishara, milio 21 ya bunduki, pembe, na ving'ora.
  4. Kiashiria. Hii ni aina ya mawasiliano ambayo inatumia alama za kidini, hadhi, au za kujenga nafsi.


Sifa zisizobadilika

Umbali. Umbali mtu mmoja anaosimama kutoka kwa mtu mwingine kwa kawaida huwasilisha ujumbe fulani. Katika baadhi ya tamaduni hii ni ishara ya mvuto, na kwa wengine inaweza kuonyesha hadhi au umuhimu wa ujumbe unaopitishwa.

Namna ya kujiwasilisha. Watu wanaweza kujiwasilisha kwa njia mbalimbali: uso kwa uso, ubavu kwa ubavu, au hata wakifuatana. Kwa mfano, watu walio na ushirikiano kuna uwezekano watakaa ubavu kwa ubavu na washindani wakati mwingi hutazamana.

Namna ya kukaa. Kwa kawaida mtu anaweza kuwa amelala chini, ameketi, au amesimama. Hivi si vipengele vya mkao vinavyowasilisha ujumbe. Je, sisi tunatembea kwa kujikokota au tumesimama wima? Tunakunja miguu au mikono yetu? Njia kama hizi za kukaa huwasilisha kiwango cha urasmi na kiwango cha mapumziko katika mawasiliano.

Mgusano wa kimwili. Kusalimiana kwa mikono, kugusana, kushikana, kukumbatiana, kusukumana, au kupiga kofi mgongoni, haya yote huwasilisha ujumbe. Huwa yanaashiria urafiki au hisia za (au ukosefu wa) mvuto.


Sifa Badilifu

Ishara za uso. Tabasamu, kukunja uso, kuinua nyusi, piga miayo, na kukenua, hivi vyote huwasilisha habari. Ishara za uso hubadilika mara kwa mara wakati wa mawasiliano na hufuatiliwa sana na mpokeaji. Kuna ushahidi kuwa maana ya ishara hizo inaweza kuwa sawa katika tamaduni mbalimbali.

Ishara. Mojawapo ya ishara zinazotumiwa, lakini zisizoeleweka, ni vidokezo katika mwondoko wa mkono. Watu wengi hutumia mara kwa mara miondoko ya mkono wanapoongea. Wakati baadhi ya ishara (mfano, kukunja ngumi) zina maana bia, nyingi za ishara huwa kila mtu anajifunza kibinafsi na zina upekee.

Kutazama. Kipengele kikubwa cha mawasiliano ya kijamii ni kutazamana macho. Kipengele hiki kinaweza kuwasilisha hisia, ashiria wakati wa kuzungumza au kuacha kuzungumza, au chuki. Marudio ya kutazamana yanaweza kuonyesha aidha shauku au uchovu.

Mawasiliano ya kutazama

[hariri | hariri chanzo]

Mawasiliano ya kutazama, kama jina linavyodokeza, ni mawasiliano kwa njia ya vielelezo. Ni kupitisha mawazo na habari katika aina ambazo zinaweza kusomwa au kutazamwa. Kimsingi yanahusishwa na vipimo vya aina mbili, na yanahusisha: ishara, tipografia, uchoraji, miundo ya grafia, mchoro, rangi na rasilimali za kielektroniki. Mawasiliano hayo hutegemea tu kutazama. Ni aina ya mawasiliano ilijengwa kwenye wazo kwamba ujumbe unaoonekana ukiunganishwa na maandishi huwa na uwezo mkubwa wa kutaarifu, kuelimisha au kumshawishi mtu. Ni mawasiliano kwa kuwasilisha taarifa kupitia vielelezo.

Tathmini ya muundo mzuri wa kutazamwa hujikita kwenye kupima ufahamu na watazamaji, wala si ujumi au upendeleo wa kisanii. Hakuna kanuni bia za uzuri na ubaya. Kuna njia mbalimbali za kuwasilisha taarifa kwa kutazama, kama vile kutumia ishara, miondoko ya mwili, video na TV. Hapa, lengo liko kwenye kuwasilisha matini, picha, michoro na kadhalika, zikiunganishwa kwenye maonyesho ya tarakilishi. Dhana wasilisho la kutazama hutumiwa kurejelea uwasilishaji halisi wa taarifa. Utafiti wa hivi karibuni katika sehemu hii umelenga miundo ya tovuti na matumizi ya grafiti. Waundaji wa grafiti hutumia mbinu za mawasiliano ya kutazama katika kazi yao.

Aina nyingine za mawasiliano

[hariri | hariri chanzo]

Aina nyingine za mawasiliano maalumu ni kama vile:

Mawasiliano ya mdomo

[hariri | hariri chanzo]

Mawasiliano ya mdomo ni mchakato ambapo habari hupitishwa kutoka kwa msemaji hadi kwa msikilizaji kupitia mdomo, lakini vielelezo vinaweza kutumiwa kusaidia katika mchakato huu. Msikilizaji anaweza kuwa mtu mmoja, kikundi au hata hadhira. Kuna aina chache za mawasiliano ya mdomo: majadiliano, hotuba, mawasilisho, n.k. Hata hivyo, mara nyingi wakati unawasiliana ana kwa ana miondoko ya mwili na toni ya sauti yako huwa na athari kubwa kuliko maneno halisi unayoyasema. Kulingana na utafiti wa hapo juu unaweza kuona kwamba maudhui au neno unalolitumia silo litakaloamua sehemu ya mawasiliano mazuri. "Jinsi unavyowasilisha ujumbe" huwa na athari kubwa kwa msikilizaji. Ni lazima unase umakini wa hadhira na uhusiane nao. Kwa mfano, watu wawili wanaosema kichekesho, mmoja wao anaweza kuifanya hadhira kuangua kicheko kutokana na miondoko mizuri ya kimwili na toni ya sauti. Hata hivyo, mtu wa pili anayewasilisha kichekesho kile kwa maneno yale yale anaweza kuifanya hadhira itazamane.

Katika mawasiliano ya mdomo, inawezekana kutumia vielelezo ili kukusaidia kuwasilisha habari kwa usahihi zaidi. Mara nyingi, tunaweza kutumia 'PowerPoint' katika mawasilisho yanayohusiana na hotuba zetu ili kuwezesha au kuboresha mchakato wa mawasiliano. Ingawa, hatuwezi kuwasiliana kwa kutumia vielelezo tu kwa sababu sisi hatutakuwa tukizungumza kuhusu mawasiliano ya mdomo tena.

Maumbo ya mawasiliano

[hariri | hariri chanzo]
Mipango mikuu ya Mawasiliano
Mipango ya kodi za mawasiliano

Mawasiliano kwa kawaida hufafanuliwa kwa kuzingatia mitazamo michache mikuu: Ujumbe (mambo ya aina gani yanayosemwa), chanzo / mtumaji / Msemaji / Mfumbaji (ambaye anatuma), aina (ujumbe ni wa aina gani), njia (unatumwa kupitia njia gani), unapokwenda / mpokeaji / lengo / mpokeaji (anayepokea ujumbe), na lengo au kipengele cha kipragramatiki. Kati ya vikundi, mawasiliano yanahusisha vitendo vinavyotunukia maarifa na tajriba, kupatia mawaidha na amri, na kuuliza maswali. Matendo haya yanaweza kuchukua sura nyingi, katika mojawapo ya njia mbalimbali za mawasiliano. Sura hizi hutegemea uwezo wa kikundi kinachowasiliana. Pamoja, maudhui na sura za mawasiliano kukamilisha ujumbe unaotumwa mahali. Mpokeaji anayelengwa anaweza kuwa msemaji mwenyewe, mtu mwingine au kiumbe kingine, kikundi kingine (kama vile shirika au kikundi cha viumbe).

Mawasiliano yanaweza kuonekana kama mchakato wa kusambaza habari unaoongozwa na viwango vitatu vya sheria za elimu ishara:

  1. Kiwango cha kisintaksia (sifa rasmi za ishara na viashiria),
  2. Kiwango cha kipragmatiki (kinahusika na mahusiano kati ya ishara / maneno na watumiaji wake) na
  3. Kiwango cha kisemantiki (utafiti wa uhusiano kati ya ishara na viashiria na yale vinayowasilisha).

Kwa hiyo, mawasiliano ni mwingiliano wa kijamii ambapo angalau vitu au watu wawili wanaotagusana hutumia seti moja ya ishara na seti moja ya kanuni za kielimu ishara. Sheria hizi zinazozingatiwa wakati mwingine huwa zinapuuza mawasiliano ambayo hutokea bila kupangiwa, yaliwemo mawasiliano ya mtu na nafsi yake kupitia kwa shajara au mazungumzo-nafsi, yote ambayo ni matukio ya sekondari yaliyofuatia kujifunza lugha katika maingiliano ya kijamii.

Katika mfano rahisi, habari au maudhui (mfano ujumbe katika lugha asilia) hutumwa katika njia fulani (kama lugha ya mazungumzo) kutoka kwa mtumaji / msemaji / mfumbaji kwa mahali maalum / mpokeaji / mfumbuaji. Katika njia changamano zaidi, msemaji na mpokeaji huwa wameunganishwa kwa wakati mmoja. Mfano mmoja wa mawasiliano ni kama tendo usemi. Namna ya kutafsiri ujumbe ya msemaji inaweza kuwa tofauti na ya msikilizaji kulingana na desturi na tamaduni za eneo walilomo, au jinsia; mambo ambayo yanaweza kuathiri ujumbe uliokusudiwa. Uwepo wa kelele za mawasiliano katika njia inayotumiwa (ikiwa ni hewa, katika kesi hii), mapokezi na ufumbuaji wa ujumbe unaweza kuathiriwa, hivyo basi tendo usemi linaweza kutofikia matokeo yaliyotarajiwa. Tatizo moja la mfano huu wa kupakia-kutuma-kupokea-kupakua ni kwamba mchakato wa kupakia na kupakua huashiria kwamba mtumaji na mpokeaji, kila mmoja ana kitu kinachofanya kazi kama kitabu cha kodi , na kwamba vitabu hivi viwili vya kodi vinafanana kwa kiasi ikiwa si kabisa. Ingawa kitu kama vitabu vya kodi kimetajwa na mfano huu, havijawakilishwa kwenye sehemu yoyote ya mfano huu, jambo ambalo linaibua matatizo mengi ya kuelewa.

Nadharia za urekebishaji-pamoja huelezea mawasiliano kama mchakato wa ubunifu na unaobadilika badilika, unaoendelea wala si kubadilishana tu kwa habari. Mwanataaluma wa vyombo vya habari kutoka Kanada Innis Harold alikuwa na nadharia kwamba watu hutumia njia mbalimbali kuwasiliana na njia watakayochagua kutumia itawapa uwezekano tofauti wa kuumba na kudumisha jamii (Wark, McKenzie 1997). Mfano wake maarufu wa kufafanua haya ni kutumia Misri ya kale na kuangalia vile wao walijijenga wenyewe nje ya vyombo vya habari kwa aina tofauti za mawe na mafunjo. Mafunjo ndiyo aliyoyaita 'Kufunga Nafasi (Space Binding)'. Kufunga huku kuliwezesha kupitishwa kwa maandishi kutoka sehemu moja hadi nyingine na kuwezesha kufanyika kwa kampeni za kijeshi za mbali na utawala wa kikoloni. Mengine ni jiwe na 'Kufunga Wakati (Time Binding)', kupitia ujenzi wa mahekalu na piramidi, wanaweza kuendeleza mamlaka yao kizazi hadi kizazi, kwa kupitia njia hii ya kupitisha habari, wanaweza kubadilika na kuumba ya mawasiliano katika jamii yao (Wark, McKenzie 1997).

Bila mawasiliano ya watu

[hariri | hariri chanzo]

Mawasiliano katika mingi ya mitazamo yake hayajajifungia tu kwa binadamu, au hata kwa sokwe. Kila mabadilishano ya habari kati viumbe vilivyo hai - yaani kubalishana kwa ishara kunakohusiha mtumaji na mpokeaji walio hai - kunaweza kuchukuliwa kama njia ya mawasiliano. Kwa hivyo, kuna uwanja mpana wa mawasiliano ya wanyama, ambayo yanahusisha mengi ya masuala katika ethnolojia. Pia wanyama waasili kama mwamba tumbawe wanaweza kuwasiliana. [5] Katika ngazi ya kimsingi zaidi, kuna kupatiana ishara kati ya seli, mawasiliano ya seli, na mawasiliano ya kemikali kati ya viumbe asili kama bakteria, [6] na miongoni mwa mimea na himaya za kuvu. Michakato hii yote ya mawasiliano huhusisha mitagusani inayoshirikisha ishara zilizo na ratibu bainifu mbalimbali.

Mawasiliano ya wanyama ni tabia yoyote kwa upande wa mnyama mmoja iliyo na athari ya sasa au baadaye kwenye tabia ya mnyama mwingine. Bila shaka, mawasiliano ya binadamu yanaweza kujumlishwa kama mawasiliano ya wanyama yaliyoendelezwa. Utafiti wa mawasiliano ya wanyama, uitwao zoosemiotiki (zoosemiotics), tofauti na anthroposemiotiki (anthroposemiotics, utafiti wa mawasiliano ya binadamu) umechangia pakubwa katika ukuzaji wa etholojia, biolojia-jamii na masomo ya uwezo wa mnyama wa kutambua.

Jambo hili ni dhahiri kwani binadamu huwa wanaweza kuwasiliana na wanyama, hasa pomboo na wanyama wengine ambao hutumika katika sarakasi. Hata hivyo, hawa wanyama hulazimika kujifunza njia za kipekee za mawasiliano. Mawasiliano ya wanyama, na haswa kuelewa ulimwengu wa mnyama kwa ujumla, ni taaluma inayokua kwa kasi, na hata katika karne ya 21 kufikia sasa, uelewa mwingi wa hapo awali kuhusiana na nyanja mbalimbali kama vile matumizi ya kiishara ya jina, hisia za wanyama, utamaduni, kujifunza kwa wanyama na hata tabia za kingono, zilizofikiriwa kwa muda mrefu kuwa zimeeleweka vizuri, zimebadilika pakubwa.

Mimea na kuvu

[hariri | hariri chanzo]

Miongoni mwa mimea, mawasiliano huonekana ndani ya mmea wenyewe, yaani, ndani ya na kati ya seli za mimea, kati ya mimea ya spishi moja au spishi zinazohusiana, na kati ya mimea na viumbe visivyo hai, hasa katika sehemu ya mizizi. Mizizi ya mimea huwasiliana na bakteria za rhizobia, na kuvu pamoja na wadudu walio kwenye ardhi. Mitagusano hii sambamba inayohusisha ishara na inayoongozwa na kanuni za kisintaksia, kipragmatiki na kisemantiki hutokea kwa sababu ya "mfumo wa neva" wa mimea uliogatuka.

Maana asilia ya neno nyuro katika Kigiriki ni "nyuzinyuzi za mboga" na kama utafiti wa hivi karibuni unavyoonyesha, mengi ya mawasiliano ya ndani ya mmea hufanana na ya nyuro. [7] Mimea pia kuwasiliana kupitia kwa mivuke katika kisa cha tabia za wakati wa mashambulizi na wanyama wala mimea, ili kuonya mimea jirani. Sambamba na hayo, mimea hiyo hutoa mivuke ya kuvivutia vimelea ambavyo huwashambulia wale wanyama. Katika hali ya dhiki mimea inaweza kubadilisha kodi ya kinasaba iliyorithi kutoka kwa wazazi wao na kurudi kwa ile ya mababu zao. [8]

Kuvu huwasiliana ili kuratibu na kupanga ukuaji wao wenyewe na maendeleo yao kama vile malezi ya seli zake na sehemu za kuota. Aidha, kuvu huwasiliana spishi zinazofanana au kuhusiana pamoja na spishi zisizokuvu katika mitagusano ya kimfaano, haswa na bakteria, 'unicellular eukaryotes' , mimea na wadudu. Kemikali za kisemiotiki zinazotumiwa huwa za asili ya kibayotiki na hufanya kuvu kuonyesha athari maalum, ambapo, katika tofauti wakati hata huo kemikali za molekuli huwa si sehemu ya ujumbe wa biotiki unaosababisha msisimko wa viumbe-kuvu. Ina maana kuwa, kuvu zinaweza kutambua tofauti katika molekuli ambazo ni sehemu ya ujumbe wa kibayotiki au kutokuwepo kwa sifa hizi. Hadi sasa kuna molekuli tano tofauti na za msingi zinazojulikana ambazo huratibisha ruwaza tofauti za kitabia kama vile 'nyuzi za hisia', kuzaana, ukuaji, usababishaji wa magonjwa. Uratibu wa tabia na uzalishaji wa vitu kama hivi unaweza tu kufikiwa kupitia michakato fasili: ya kibinafsi au isiyo ya kibinafsi, kiashiria cha kibiotiki, ujumbe wa kibiotiki kutoka kwa spishi zinazofanana, zinazohusiana au zisizohusiana, au hata "kelele", yaani, molekuli zinazofanana lakini hazina ujumbe wa kibiotiki. [9]

Mawasiliano kama taaluma ya kiakademia

[hariri | hariri chanzo]

Mawasiliano kama taaluma ya kiakademia, ambayo wakati mwingine huitwa "komunikolojia," [10] inahusiana na njia zote tunazozitumia kuwasiliana, hivyo basi inahusisha sehemu kubwa ya utafiti na maarifa. Taaluma ya mawasiliano inahusisha mawasiliano ya kimaongezi na yasiyo ya kimaongezi. Mkusanyiko wa maarifa kuhusu mawasiliano umewakilishwa na kufafanuliwa katika vitabu, machapisho ya kielektroniki, na majarida ya kiakademia. Katika majarida, ripoti za kitafiti ndizo matokeo ya tafiti ambazo ni msingi wa uelewa, unaoendelea kupanuka, wa jinsi sisi wote tunavyowasiliana.

Mawasiliano hufanyika katika ngazi tofauti (hata kwa tendo moja), katika njia mbalimbali, na kwa viumbe wengi, na vilevile kwa mashine fulani. Baadhi ya taaluma za utafiti , ikiwa siyo zote, hutenga sehemu ya mafunzo yake kwa mawasiliano, hivyo basi wakati wa kuzungumza kuhusu mawasiliano, ni muhimu sana kuwa na uhakika kuhusu nyanja ya mawasiliano inayozungumziwa. Ufafanuzi wa mawasiliano hutofautiana sana, baadhi yake ukitambua kwamba wanyama wanaweza kuwasiliana na wenzao na binadamu pia, na baadhi ni finyu zaidi, ukihusisha binadamu katika mitagusano ya kibinadamu iliyo na maana.

Umuhimu wa mawasiliano

[hariri | hariri chanzo]

Hakuna linaloweza kufanikiwa pasipo mawasiliano. Mawasiliano ni kati ya nafsi na nafsi – hivyo nafsi zisipokuwa na mawasiliano ina maana miili inayobeba nafsi hizo haiwezi kushirikiana kwa lolote. Kitu kimoja ambacho ni kikwazo cha mawasiliano ni woga. Ndio unaokufanya usiwasiliane na fulani, usiwe na ushirika naye. Woga huo ndio unaosababisha usipate usaidizi toka popote pale.

  1. Schwartz, Gary E.; Simon, William L.; Carmona, Richard (2008). The Energy Healing Experiments. Simon & Schuster. uk. 129. ISBN 0743292399. All communication is a process of exchanging energy and exchanging information. {{cite book}}: Check |isbn= value: checksum (help)
  2. "communication". office of superintendent of Public instruction. Washington. Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo 2009-11-19. Iliwekwa mnamo 14 Machi 2008. {{cite web}}: Unknown parameter |dateformat= ignored (help)
  3. Mehrabian na Ferris (1967). "Inference of Attitude from Nonverbal Communication in Two Channels". Katika: The Journal of Counselling Psychology Vol.31, 1967, pp.248-52.
  4. Warwick, K, Gasson, M, Hutt, B, Goodhew, I, Kyberd, P, Schulzrinne, H na Wu, X: "Thought Communication and Control: A First Step using Radiotelegraphy", IEE Proceeedings on Communication, 151 (3), pp.185-189, 2004
  5. Witzany G, Madl P. (2009). Biocommunication of corals. International Journal of Integrative Biology 5 (3): 152-163.
  6. Witzany G (2008). Bio-Communication of Bacteria and their Evolutionary Roots in Natural Genome Editing Competences of Viruses. Open Evolution Journal 2: 44-54.
  7. Baluska, F.; Marcuso, Stefano; Volkmann, Dieter (2006). Communication in plants: neuronal aspects of plant life. Taylor & Francis US. uk. 19. ISBN 3540284758. ...the emergence of plant neurobiology as the most recent area of plant sciences. {{cite book}}: Check |isbn= value: checksum (help)
  8. Witzany, G. (2006 Plant Communication from Biosemiotic Perspective. Plant Signaling na Behavior 1 (4): 169-178.
  9. Witzany, G. (2007 Applied Biosemiotics: Fungal meddelande. Katika: Witzany, G. (Ed). Biosemiotics in Transdisciplinary Contexts. Helsingfors, Umweb, uk. 295-301.
  10. "Nakala iliyohifadhiwa". Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo 2009-09-23. Iliwekwa mnamo 2009-11-23.