Maulid
Maulid (pia: maulidi, kwa kirefu: Maulid an-Nabii) ni sikukuu ya dini ya Uislamu ya kuadhimisha kuzaliwa kwake Mtume Muhammad takriban mwaka 570 BK.
Neno lenyewe ni la asili ya Kiarabu kutokana na مولد النبي , maulid an-nabi, au ميلاد النبي , milaad an-nabi). Sikukuu inafuata kalenda ya Kiislamu. Waislamu wa dhehebu la Sunni husheherekea tarehe 12 Rabi'-ul-Awwal kwa mujibu ya kalenda ya Kiislamu ya Alhijria na Waislamu wa dhehebu la Shia husheherekea tarehe 17 Rabi'-ul-Awwal.
Wataalamu wa historia wengine wanasema ya kwamba sherehe ya Maulid imeanzishwa mnamo karne ya 12 BK. Kuna Waislamu kadhaa wanaokataa sherehe hiyo kwa sababu hakuna sunna wala hadith ya Muhammad mwenyewe kuhusu kusheherekea maulid yake. Lakini kwa ujumla ni sikukuu inayopendwa sana na Waislamu wengi duniani. Misri maulid ni kati ya sikukuu za Kiislamu zinazokumbukwa sana na Waislamu. Katika Afrika ya Mashariki sherehe ya maulid huko Lamu imejulikana hasa ikivuta wageni kutoka pande zote za Afrika ya Mashariki hadi Uarabuni.
Kati ya desturi ni mikutano, kusikia mashairi juu ya maisha ya mtume a mengine.
Tarehe za Maulid katika kalenda ya Gregori
[hariri | hariri chanzo]Maulid kama vile sikukuu zote za Kiislamu inafuata kalenda ya Kiislamu ambayo ni kalenda ya mwezi. Kwa sababu hiyo tarehe yake hubadilikabadilika katika kalenda ya Gregori iliyoenea kimataifa.
Kalenda ya kiislamu hubadilika kulingana na kuandama kwa mwezi.
Zifuatazo ni tarehe za maulid kwa ajili ya miaka 2006 - 2021. Tarehe ya kwanza ni ile ya Wasunni (12 Rabi'-ul-Awwal) na tarehe ya pili katika mabano ni ile ya Washia (17. Rabi'-ul-Awwal). Tarehe hizo zinaweza kuwa tofauti na tarehe halisi kwa sababu kuna tofauti kati ya nchi na vikundi vya Waislamu jinsi gani kukubali kuhusu mwanzo wa miezi.
- 2006: 12 Aprili, (17 Aprili)
- 2007: 31 Machi, (5 Aprili)
- 2008: 20 Machi, (25 Machi)
- 2009: 9 Machi, (14 Machi)
- 2010: 26 Februari, (3 Machi)
- 2011: 15 Februari, (20 Februari)
- 2012: 4 Februari, (9 Februari)
- 2013: 24 Januari, (29 Januari)
- 2014: 13 Januari, (18 Januari)
- 2015: 2 Januari, (7 Januari)
- 2016: 22 Desemba, (27 Desemba)
- 2017: 11 Desemba, (16 Desemba)
- 2018: 30 Novemba, (5 Desemba)
- 2019: 19 Novemba, (24 Novemba)
- 2020: 8 Novemba, (13 Novemba)
- 2021: 28 Oktoba, (2 Novemba)
Viungo vya nje
[hariri | hariri chanzo]- (Kiingereza)Islamic Holy Days Archived 18 Aprili 2006 at the Wayback Machine.
- (Kiingereza)Mawlid
- Video Russian Mawlid
- Turkish Mawlid Archived 30 Septemba 2018 at the Wayback Machine.