Nenda kwa yaliyomo

Dizasta Vina

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Dizasta Vina
Dizasta Vina akiwa katika pozi - Oktoba 2023
Taarifa za awali
Jina la kuzaliwaEdger Vicent Mwaipeta
Pia anajulikana kamaThe Black Maradona, Professor Tungo, Fundi Vina
Amezaliwa17 Februari 1993 (1993-02-17) (umri 31)
Iringa, Tanzania
ChimbukoMbeya, Tanzania
Aina ya muzikiHip hop
Kazi yakeRapa, Mtunzi, Mshairi, Mtayarishaji wa rekodi
AlaSauti, Kinanda
Miaka ya kazi2012 - sasa
StudioPanorama Authentik
Ameshirikiana naBaraka the Prince, G Nako, One The Incredible, Nikki Mbishi, Nash MC, JCB wa Watengwa

Edger Vicent Mwaipeta (anafahamika zaidi kwa jina la kisanii kama Dizasta Vina; amezaliwa Iringa, Tanzania, 17 Februari 1993) ni msanii wa muziki wa Hip Hop na mtayarishaji wa muziki kutoka nchini Tanzania. Ni mmoja kati ya watu walioanzisha kundi la Panorama Authentik.[1] [2]

Ni msanii ambaye muundo wa mashairi yake unajumuisha usimuliaji wa matukio na hadithi za maisha halisi ya jamii aliyotokea. Tungo zake zinasifika kwa kuelimisha na kugusa mausula ya kijamii kama vile malezi, maradhi, siasa, umasikini, elimu, haki na usawa, uraibu wa madawa ya kulevya na masuala mengine ndani na nje ya jamii na taifa lake na ulimwengu mzima kwa jumla.[3]

Mwaka 2004 mama yake alimpeleka kwenye tamasha la mkesha wa mwaka mpya, Dhando Hall Mbeya. Mike Tee na Mr Blue walitumbuiza usiku huo. Dizasta alishangazwa na namna Mr Blue alivyoweza kutumbuiza mbele ya watu wengi kiasi kile na katika umri mdogo. Tangu hapo alianza kutamani kuwa kama yeye kwenye wakati ule. Kutokea hapo wazo la kuwa mwanamuziki liliishi kichwani mwake.

Kwanzia mwaka 2009 alianza kushiriki kwenye majukwaa mbalimbali ya Hip Hop. Mwaka 2010 alishiriki kwenye "Hot Fm Freestyle Battle", mashindano ya mitindo huru yaliyoandaliwa na redio ya matangazo ya kiingereza ya Hot Fm mkoani Iringa. Akiwa bado anatumia jina lake halisi, dada ambaye alikuwa mmoja wa waandaaji na watangazaji wa mashindano hayo Dj Divanji alimpa jina la "Disaster" kutokana na uwezo wake wa kuchana. Jina lilipata umaarufu kwa mashabiki na aliamua kutumia jina hilo kukumbuka huo wakati. Aliongeza neno "Vina" kwenye jina lake la kisanii kutunza heshima ya kaka yake wa shuleni Adam Kasim aliyekuwa anajiita "Mavina". Adam ndiye aliyemfundisha vitu mbalimbali vinavyohusiana na uandishi wa mashairi ya hip hop.

Mwaka 2012 alishiriki mashindano ya uchanaji wakati wa tamasha la uzinduzi wa Santuri 5 za Hip Hop Tamaduni Muzik pale New Msasani Club na alikuwa miongoni mwa washindi watano (ikiwa ni pamoja na Dan General, Kinya Mistari, Bale boy na Shua mkuu) waliofanikiwa kujiunga na familia ya Tamaduni Muzik.[4][5] Mwaka huohuo alitoa wimbo wake wa kwanza uliokwenda kwa jina "Harder", ulitengenezwa na More Mocco na Laheel Paps.[6]

Mnamo mwaka wa 2017, alitoa kandamseto yake ya kwanza "The Wonderboy Mixtape". Aliachia nyimbo kadhaa na kufanikiwa kutoa albamu yake ya kwanza "JESUSta" mwaka wa 2018. Mnamo tarehe 27 Desemba 2020, alitoa albamu yake ya pili "The Verteller".[7] Kando na kutoa nyimbo, Dizasta amekuwa akifanya utayarishaji wa nyimbo zake, hii ni baada ya kuamua kukaa chini na kuanza kusoma namna ya kutayarisha muziki na kufanya uhandisi wa sauti.

Maisha ya awali

[hariri | hariri chanzo]

Dizasta Vina alizaliwa na jina la Edger Vicent Mwaipeta mnamo tarehe 17 Februari 1993 katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa. Wakati huo, wazazi wake walikuwa wakiishi Mtaa wa Kota, Kata ya Mlandege, Iringa. Ni mtoto wa pili kuzaliwa katika familia yao na ni mwanaume pekee akiwa na dada zake wawili. Kiasili, Dizasta anatoka mkoa wa Mbeya, ambapo yeye ni Mnyakyusa. Hata hivyo, alizaliwa Iringa Mjini na mwaka 2003, akiwa na umri wa miaka 10, familia yake ilihamia jijini Dar es Salaam kwa sababu za kikazi. Aliendelea na masomo yake ya elimu ya msingi jijini humo.

Dizasta Vina akikabidhiwa zawadi na Salma Kikwete kama mwanafunzi bora - White Lake High School, 2008.

Baada ya kuhamia Dar es Salaam mwaka 2003, alijiunga na Shule ya Msingi Jeshini, iliyopo Ukonga. Mwaka mmoja baadaye, alihamishiwa Shule ya Msingi Kimanga, iliyopo Tabata Kimanga, na alihitimu elimu ya msingi mwaka 2006. Mwaka 2007, alijiunga na shule binafsi ya sekondari ya White Lake High School, Changanyikeni, Dar es Salaam, na baadaye alihamishiwa shule ya Southern Highlands Secondary School, Soweto, Mbeya, ambako alihitimu masomo yake ya sekondari mwaka 2010. Aliendelea na kidato cha tano katika shule ya Kigoma High School, mkoani Kigoma, lakini alisoma kwa muda wa miezi minne tu kabla ya kuhamia shule ya Mbeya High School, ambako alimalizia masomo yake ya sekondari. Mwaka 2013, alijiunga na Chuo cha Usimamizi wa Fedha (Kiingereza: Institute of Finance Management (IFM)) kilichopo jijini Dar es Salaam na kuchukua shahada ya awali ya uhasibu.

Kwenye umri wa mwanzo wa kujielewa (kwanzia miaka 11 na kuendelea), Dizasta aliishi Tabata. Tabata ya miaka ya 2004 kuja mpaka 2010 ulikuwa ni mji wa maisha ya chini ya mswahili. Kama inavyofahamika, maisha ya chini ya mswahili huarika uchafu. Kipindi hicho aliona wachache waliomtangulia wakifanikiwa na kuondoka mji ule na wengi wakianguka kwenye uhalifu, ulevi na matumizi ya madawa ya kulevya. Kuishi kwenye mazingira yale kulimpa nafasi ambayo wengi hawana. Nafasi ya kuona kwa mifano pande mbili za sarafu za peponi na gizani. Mazingira yale yalimpa maudhui kwenye kazi zake. Albumu yake ya The Verteller na A Father Figure ni shuhuda kutoka mazingira aliyokulia.

Kwa muda mrefu, Dizasta amekuwa akiishi Dar es Salaam, ingawa mara kwa mara husafiri kwenda Majengo, Mbeya, nyumbani kwao asili, ambako wazazi wake wanatokea. Muziki ni sehemu ya maisha yake tangu akiwa na umri mdogo, familia yake walikuwa waimbaji wa kwaya kanisani na wengine ni wanakwaya mpaka sasa.

Kazi ya muziki

[hariri | hariri chanzo]
Dizasta Vina akitumbuiza katika tamasha la "Hip Hop Asili Festival" huko Bagamoyo, Tanzania — mnamo tarehe 26 Juni, 2023.

Dizasta Vina amezaliwa katika familia inayopenda muziki na alianza kufuatilia muziki tangu akiwa na umri mdogo. Msukumo wa kuupenda muziki aliupata kutoka kwa familia yake. Mama yake alikuwa mwimbaji wa kwaya kanisani na pia kwa vipindi tofauti dada zake walijiunga na uimbaji wa kwaya. Wakati anakua, Vina alijulikana mtaani kwa kukariri nyimbo za wanamuziki mashuhuri nchini Tanzania kama vile Professor Jay, Afande Sele, Juma Nature, na Solo Thang. Wakati fulani, watu walikuwa wakimpa pesa ili awaimbie baadhi ya nyimbo zilizotamba wakati huo. Alianza kutamani kuwa mchanaji baada ya kusikiliza albamu ya "Machozi Jasho na Damu" ya Professor Jay.

Dizasta vina alianza rasmi kujishughulisha na masuala ya muziki mnamo mwaka wa 2007 kwa kushiriki katika mashindano mbalimbali ya kurap ikiwa ni pamoja na SM Straight Music Freestyle Battle mwaka wa 2010 mkoani Iringa. Mashindano kama haya yalimjengea msingi wa kuwa mwanamuziki na kumpa hamasa ya kujifunza zaidi kuhusu misingi ya utamaduni wa hip hop.

Mnamo mwaka wa 2011 alikutana na mtayarishaji wa muziki, Duke Touchez. Duke alimpa mwongozo wa jinsi ya kujiunga na Tamaduni Muzik ambayo kwa kipindi hicho ilikuwa inatafuta vipaji vipya kwa ajili ya "Tamaduni Foundation". Dizasta alishiriki shindano ya kuchana lililofanyika wakati wa tamasha la kuachia santuri tano kwa mpigo ("African Son" ya Stereo, "Sauti ya Jogoo" ya Nikki Mbishi, "Mzimu wa Shaaban Robert" ya Nash MC, "Underground Legendary" ya Duke Touchez na "Mathematrix" ya Songa na Ghetto Ambassador).[8] Baada ya shindano hilo alifanikiwa kujiunga rasmi na Tamaduni Muzik. Alianza kupata umaarufu mnamo mwaka wa 2012, alipotoa wimbo wake wa kwanza 'Harder'.[9]

Mwaka wa 2013, Dizasta alitoa wimbo ulioitwa "Tega sikio", kisha akatoa "Goli la ushindi", "Nyumba Ndogo" na "Sister". Dizasta alishirikishwa kwenye albamu ya "Underground Project" ya mtayarishaji wa muziki anayefahamika kwa jina la AK 47, kwenye wimbo uliokwenda kwa jina la "Heavyweight" alishirikiana na mwanamuziki wa kike, Tifa Flows. Mwaka huo huo alishirikishwa katika albamu ya "Upande wa pili wa sarafu" ya mtayarishaji wa muziki Abby Mp, kazi ya kilinge ya Duke Touchez, albamu ya "Kiutu Uzima" ya msanii Kadgo, Kandamseto ya "Slow Jams" ya mtayarishaji wa muziki - Innocent Mujwahuki, "Tamaduni Foundation" ya Ngwesa na "Representing Africa Popote" ya One the Incredible.

Dizasta akiwa anaendelea na masomo ya chuo kikuu alijifunza mambo madogo madogo ya kuwa mwanamuziki wa kujitegemea. Kufikia mwaka wa 2015, Vina alikuwa maarufu nchini Tanzania baada ya kutoa wimbo wa ‘Kijogoo’ na ‘Siku Nikifa’. Mwaka 2017 alitoa kandamseto yake ya kwanza iliyokwenda kwa jina la "The Wonderboy Mixtape".[10] Kandamseto hii ilivuta usikivu wa wadau wengi wa muziki na alianza kuzungumziwa kupitia media mbalimbali kama mmoja wa wasanii bora wa kizazi kipya na mtunzi mahiri wa nyimbo za masimulizi.[11] Mnamo 14 Februari 2018, Dizasta alipata mwaliko kwenye "Dakika 10 za Maangamizi" kipindi kidogo ndani ya kipindi cha Planet Bongo cha East Africa Radio. Iliripotiwa kuwa kipindi chake cha mitindo huru ni mojawapo ya kipindi bora zaidi kwenye mfululizo wa kipindi hicho.[12]

2018: Jesusta

[hariri | hariri chanzo]

Desemba mwaka wa 2018, Dizasta Vina alitoa albamu yake ya kwanza iliyoitwa "Jesusta". Albamu hiyo yenye nyimbo 20 imeshirikisha wasanii wengine ikiwa ni pamoja na Nikki Mbishi, Shaolin Senetor, Bokonya, Kinya, Motra the Future, Boshoo na Jeff Mduma. Albamu ilivuta hisia za wapenzi wengi wa muziki wa hip hop kote nchini na ilijumuisha nyimbo maarufu kama: "The Lost One", "Nobody is Safe", " Kanisa"[13], na "Hatia". Wimbo wa "Kikaoni" ambao aliutayarisha mwenyewe uliingia katika chati za vituo kadhaa vya redio jijini Dar es Salaam na kote Tanzania.[14]

2020:The Verteller

[hariri | hariri chanzo]
Makala kuu: The Verteller

"The Verteller" albamu ya pili ya Dizasta Vina ilitolewa tarehe 27 Desemba 2020 ilitolewa kupitia Panorama Authentik na utayarishaji wake ulishughulikiwa na Ringle Beatz (ambaye pia amesimama kama mtayarishaji mkuu), Cjmoker na Jcob.

Dizasta alirekodi albamu hii kati ya mwaka 2019 na 2020. The Verteller ina jumla ya nyimbo 20 kama mtangulizi wake na imeshirikisha wasanii wengine kutoka nchini Tanzania ikiwa ni pamoja na Tk Nendeze, Adam ShuleKongwe, Bokonya, Wakiafrika, Nasra Sayeed na Dash. Albamu ilipokelewa vyema na mashabiki na wapenzi wa muziki. Nyimbo kama "Ndoano", " The Confession of a Mad Man", "Wimbo usio bora", " Kesho" na "Muscular Feminist" zilimletea umaarufu zaidi wa kitaifa na ufuasi mkubwa wa mashabiki.[15]

Kutayarisha muziki

[hariri | hariri chanzo]
Dizasta Vina akiwa katika studio za Panorama Authentik jijini Dar es Salaam, Tanzania— mnamo tarehe 17 Februari, 2018.

Miaka ya karibuni, Dizasta amekuwa akitayarisha muziki wake mwenyewe, hii ni baada ya kuamua kukaa chini na kuanza kusoma jinsi ya kutayarisha muziki na kufanya uhandisi wa sauti. Baadhi ya nyimbo zake mashuhuri alizotayarisha mwenyewe ni pamoja na "Fallen Angel" iliyotoka tarehe 23 Julai 2016, "Kanisa" iliyotoka 13 Novemba 2016 na "The Lost One" iliyotoka Aprili 2017.

Uwezo wake mkubwa kama mtayarishaji ulianza kuonekana kupitia mfululizo wa nyimbo zake kama vile "Hatia", "Nobody is Safe", "Hatia II", na "Hatia III" na "Kikaoni", kibao kilicho jizolea umaarufu mkubwa kwa wapenzi wa utamaduni wa handakini kutokana na kugusa maisha ya familia na ndoa. Katika albamu ya " The Verteller" alishiriki kutayarisha wimbo wa "Tatoo Ya Asili", "A Confession of a Mad Teacher","A Confession of a Mad Son", "Ndoano", "Maabara" na "Kifo.

Anakubali kuwa amepata utaalamu na mbinu nyingi zaidi za kutayarisha muziki kutokana na kufanya kazi na watayarishaji wengine wa muziki wa Kitanzania kama Duke Touchez, Ray Teknohama na Ringle Beatz. Dizasta anaamini kuwa na taaluma ya kutayarisha muziki wake mwenyewe kuna faida kubwa kwani kunafanya afikie hisia halisi za wimbo tofauti na pale anapotafuta na kujenga mahusiano ya kimuziki na mtayarishaji mwingine.

Dizasta Vina na Tamaduni Muzik

[hariri | hariri chanzo]

Tamaduni Muzik ni jukwaa la muziki wa kujitegemea ambalo Dizasta alifanyanalo kazi kwa mafanikio makubwa. Alijiunga na Tamaduni Muzik mwaka 2012 baada ya kuwa moja ya washindi watano wa mashindano ya uchanaji yaliyoandaliwa na Tamaduni Muzik na kufanyika New Msasani Club. Duke Touchez mtayarishaji wa muziki na mwanzilishi wa M Lab Records, Tamaduni Muzik, na Hip Hop Kilinge (Kiingereza: Hip Hop cypher) alivutiwa na uwezo na uelewa wake kuhusu utamaduni wa hip hop na alifanikisha kujiunga kwake na Tamaduni Muzik. Wakati huo Tamaduni Muzik ilikuwa na wasanii kama One the Incredible, Nikki Mbishi, Stereo, Zaiid, Songa, Nash MC na wengineo.

Dizasta anasema kujiunga na Tamaduni Muzik ilimsaidia kujifunza kuwa msanii anayejitegemea. Alijifunza hatua za kutayarisha muziki, namna ya kutayarisha midundo yake mwenyewe, kujitangaza, mbinu za kusambaza muziki na namna ya kubadilisha mashabiki kuwa wateja wa kazi zake.

Kupitia Tamaduni Muzik waliweza kubadilisha na kutimiza nguzo karibia zote za hip hop zinavyotaka. Maoni ya Dizasta Vina kuhusu Tamaduni Muzik ni kwamba ndio wao waliobadilisha mtazamo na mwelekeo mzima wa muziki wa hip hop ya Tanzania. Kupitia wao, tuliweza kuona kutolewa kwa albamu kwa sana hata kwa wasanii wachanga, kutoa kandamseto, kurudisha maonesho ya hip hop kukusanya wasanii “Kilingeni” huko Msasani Club. Kifupi Tamaduni Muzik imehakikisha sanaa ya muziki wa hip hop inapata nafasi kubwa katika jamii ya Watanzania.

Migogoro

[hariri | hariri chanzo]

Mnamo Januari 2023 uliibuka mzozo kati ya Dizasta na msanii mwenzake Rapcha (msanii aliye chini ya nembo ya P. Funk Majani kwa sasa. Mzozo ulianza baada ya Rapcha kutoa wimbo unaoitwa "Story Nyingine" tarehe 31 Disemba 2022. Katika wimbo huo, Rapcha aliwazungumzia wasanii kadhaa ikiwa ni pamoja na Babu Tale, Young Lunya na Dizasta Vina.[16] Januari 9, 2023, Dizasta alimjibu kwa kutoa wimbo unaoitwa "Best Friend". Mzozo wao uliendelea baada ya Januari 12, 2023, Rapcha kutoa wimbo unaoitwa "Nyuclear Story", wimbo ambao moja kwa moja ulimlenga Dizasta. Siku nne mbele, Januari 17, 2023, Dizasta Vina alimjibu tena Rapcha kwa kutoa wimbo wa "Tribulation", Rapcha hakuja na jibu. Mnamo Juni 2023, Rapcha alipoulizwa juu ya hali ya ugomvi wake na Dizasta, alisema wawili hao hawatapatana na hawawezi kufanya kazi pamoja, hali ambayo hadi sasa imethibitika kuwa kweli.[17]

Diskografia

[hariri | hariri chanzo]

Hii ni orodha ya albamu za muziki alizotoa Dizasta Vina.

Na. Jina la albamu Mwaka Maelezo
1. THE Wonderboy Mixtape 2017 Kandamseto ya kwanza kutoka kwa Dizasta Vina.
2. Jesusta 2018 Albamu rasmi ya kwanza kutoka kwa Dizasta Vina.
3. The Verteller 2021 Albamu ya pili kutoka kwa Dizasta Vina.
  1. Frank Lachman (2024-03-25). "Dizasta Vina: The Legendary Tanzanian Hip Hop Artist who is redefining the genre with his rare and unique rhymes" (kwa American English). Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo 2024-03-27. Iliwekwa mnamo 2024-03-27.
  2. "Dizasta Vina". Music In Africa (kwa Kiingereza). 2022-11-10. Iliwekwa mnamo 2023-01-19.
  3. "Fid Q ataja Top 5 ya rapa wake bora Tanzania | East Africa Television". www.eatv.tv (kwa Kiingereza). 2023-11-29. Iliwekwa mnamo 2024-01-29.
  4. "30 days of Tanzanian hip hop: Day 11 Hip Hop Kilinge (cypher)". The Hip Hop African (kwa American English). 2014-09-11. Iliwekwa mnamo 2024-08-20.
  5. Tamadunimuzik (2012-08-11). ":::::::::TAMADUNIMUZIK::::::::::: UZINDUZI WA SANTURI 5 KWA PAMOJA". Iliwekwa mnamo 2024-08-21.
  6. "Dizasta Vina Biography, Music Career, Awards, Relationships and Net Worth ⚜ Latest music news online". mdundo.com (kwa Kiingereza). Iliwekwa mnamo 2022-07-28.
  7. "Micshariki Africa" (kwa Kiingereza). Iliwekwa mnamo 2022-07-28.
  8. Tamadunimuzik (2012-08-11). ":::::::::TAMADUNIMUZIK::::::::::: UZINDUZI WA SANTURI 5 KWA PAMOJA". Iliwekwa mnamo 2022-07-28.
  9. "Dizasta Vina: Zawadi nyingine kwa wapenda HipHop Tanzania". JamiiForums (kwa American English). Iliwekwa mnamo 2022-07-28.
  10. Frank Lachman (2024-03-25). "Dizasta Vina: The Legendary Tanzanian Hip Hop Artist who is redefining the genre with his rare and unique rhymes" (kwa American English). Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo 2024-03-27. Iliwekwa mnamo 2024-03-27.
  11. "Dizasta Vina anaweza akawa ndio best rapper Tanzania". JamiiForums (kwa American English). Iliwekwa mnamo 2022-07-28.
  12. Dakika 10 Za Maangamizi- Dizasta Vina | Planet Bongo I, iliwekwa mnamo 2022-07-28
  13. "Micshariki Africa" (kwa Kiingereza). Iliwekwa mnamo 2022-10-20.
  14. "Audiomack | Free Music Sharing and Discovery". audiomack.com (kwa Kiingereza). Iliwekwa mnamo 2022-07-28.
  15. Simulizi na sauti SNS (2024-03-25). "More deadly than the male: Clara Cleitus Luvanga – A story of a baller from Njombe" (kwa American English). Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo 2024-03-27. Iliwekwa mnamo 2024-03-27.
  16. "The beauty and ugliness of beefing to Bongo Flava showbiz". The Citizen (kwa Kiingereza). 2023-01-20. Iliwekwa mnamo 2024-04-02.
  17. "Rapcha Amjibu Dizasta Vina Kwenye Nyu'clear Freestyle ⚜ Latest music news online". mdundo.com (kwa Kiingereza). Iliwekwa mnamo 2024-04-02.

Viungo vya nje

[hariri | hariri chanzo]
Wikimedia Commons ina media kuhusu:
Makala hii kuhusu mwanamuziki fulani bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Dizasta Vina kama wasifu wake, habari za maisha au kazi yake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.