Atanasi wa Aleksandria
Atanasi wa Aleksandria anayeitwa Mkuu (pia Athanasio (Kigir. Ἀϑανάσιος Athanasios; Aleksandria, Misri, 295 hivi - Aleksandria, 2 Mei 373) alikuwa kiongozi wa Kanisa Katoliki nchini Misri, mwanatheolojia mashuhuri aliyetetea mafundisho ya Utatu dhidi ya Uario na anayeheshimiwa kama Babu wa Kanisa. Wakopti wanamhesabu kama Papa wa 20 wa Aleksandria.
Chini ya makaisari mbalimbali, kuanzia Konstantino Mkuu hadi Valens, maisha yote ya Atanasi yalihusika na juhudi kubwa za Kanisa kwa ajili ya kufafanua na kutetea imani sahihi juu ya Yesu na juu ya Utatu hata akaitwa mapema “nguzo ya Kanisa” (Gregori wa Nazianzo) dhidi ya uzushi wa Ario. Kwa ajili hiyo alistahimili kwa ushujaa kupigwa vita na wafuasi wa huyo na viongozi wa serikali waliompeleka uhamishoni mara tano.
Kwa mafundisho yake na kwa upendo wake motomoto kwa Kristo, tangu zamani anaheshimiwa na Wakatoliki, Waorthodoksi na Waorthodoksi wa Mashariki kama mtakatifu na mmojawapo kati ya mababu wa Kanisa walio muhimu zaidi. Anakumbukwa pia katika kalenda ya Waanglikana na Walutheri.
Mwaka 1568 Papa Pius V alimuongezea sifa ya mwalimu wa Kanisa.
Wote wanaadhimisha sikukuu yake kila mwaka tarehe 2 Mei[1].
Maisha
[hariri | hariri chanzo]Atanasi alizaliwa Aleksandria wa Misri mwishoni mwa karne III, wakati dhuluma za Dola la Roma dhidi ya Wakristo zilipozuwa zikielekea kilele na kikomo chake.
Alikulia katika jiji hilo, ambalo wakati huo lilikuwa likiongoza kimataifa upande wa biashara, ustaarabu na elimu.
Alipata elimu na malezi mazuri na tangu ujana wake alihusiana na wamonaki wa jangwa la Tebais, halafu miaka 356-362 aliishi monasterini.
Upande wa dini, baada ya dhuluma za serikali ya Dola la Roma kwisha, Wakristo wa Misri walikuwa na chuo muhimu cha katekesi, lakini kulikuwa pia na maelekeo ya hatari, hasa wafuasi wengi wa Gnosi, mbali na wale wa dini za jadi zilizoabudu miungu mingi.
Mwaka 319 askofu Aleksanda wa Aleksandria alimpa daraja takatifu ya ushemasi na kumfanya katibu wake. Akiwa bado shemasi, mwaka 325 alimsindikiza na kumsaidia kwenye Mtaguso I wa Nisea mwaka 325 ulioitishwa na Kaisari Konstantino Mkuu hasa kwa lengo la kujadili mafundisho ya padri wa Aleksandria, jina lake Ario, kuhusu dhati ya Yesu Kristo.
Huyo alisema Neno wa Mungu si Mwanae halisi, bali kiumbe tu, ingawa cha Kimungu kwa namna fulani. Hivyo alikataa uwezekano wa binadamu kushiriki umungu kwa njia ya Kristo.
Dhidi ya Ario, aliyefuatwa mapema na watawala na maaskofu wengi, huo Mtaguso mkuu wa kwanza ulitunga kanuni ya imani ambamo ulitumia neno la Kigiriki ὁμοούσιος (homoousios, yaani "wa dhati ileile" ya Baba), ili kukiri kwa namna wazi usawa kamili wa Mungu Baba na Mwana aliyezaliwa naye bila kuumbwa.
Atanasi akishikilia moja kwa moja msimamo huo, pengine kwa ukali, dhidi ya waliopinga uteuzi wake na dhidi ya waliokataa ungamo hilo alijivutia chuki ya Waario wa aina zote na dhuluma ya serikali iliyodai maelewano ili umoja wa dola usivunjike.
Mara baada ya kushika nafasi ya marehemu askofu Aleksanda, Atanasi alionyesha hatakubali maelewano tofauti na imani iliyoungamwa na umati wa maaskofu huko Nisea. Ushindani wake na serikali ulifikia kilele alipokataa agizo la Konstantino la kumrudisha Ario kwenye ushirika.
Atanasi alipaswa kustahimili dhuluma za serikali, hata akafukuzwa katika jimbo lake walau mara tano na kupelekwa uhamishoni tangu miaka michache baada ya kuchaguliwa Patriarki wa Aleksandria na wa Misri yote mwaka 328 (alipokuwa na umri wa miaka 30 tu) hadi mwaka 366, ambapo Kaisari alilazimishwa na umati amrudishe Aleksandria. Katika miaka 30, aliishi miaka 17 uhamishoni akiteseka kwa ajili ya imani.
Kumbe, akiwa mbali na Aleksandria, alitetea na kueneza hata Trier (leo nchini Ujerumani) na Roma (Italia) imani ya Nisea pamoja na umonaki. Ushindani wake na serikali ulifikia kilele alipokataa agizo la Konstantino la kumrudisha Ario kwenye ushirika.
Baada ya kurudishwa Aleksandria, aliendelea kuleta upatanisho ndani ya Kanisa na kulipanga upya.
Katika mapambano yake aliungwa mkono na Sinodi ya Roma ya mwaka 341 na ile ya Sardica ya mwaka 343.
Hatimaye aliona ushindi wa moja kwa moja wa imani ya kweli.
Maandishi
[hariri | hariri chanzo]Pamoja na kupatwa na vurugu nyingi maishani, Atanasi aliandika sana: hotuba na barua, lakini pia vitabu juu ya imani, historia, ufafanuzi wa Biblia, pamoja na maisha ya Kiroho. Kitabu chake maarufu kimojawapo kinahusu umwilisho wa Neno; humo aliandika kuwa Neno wa Mungu “alifanyika mtu ili sisi tuweze kufanywa Mungu”.
Lakini kitabu ambacho kilienea na kuathiri zaidi maisha ya Kanisa labda ni "Maisha ya Antoni" ambacho kilieneza umonaki haraka mashariki na vilevile magharibi.
Unagamo la Imani linaloitwa "Imani ya Athanasio" au "Quicumque vult" haikutungwa naye.
Teolojia yake
[hariri | hariri chanzo]Atanasi hakuwa mtu wa nadharia tu, bali hasa mchungaji aliyeona mapema hatari iliyofichika katika uzushi wa Ario, yaani kurudia Upagani wa Kigiriki. Hamu yake ilikuwa kulinda kikamilifu “mapokeo, mafundisho na imani ya Kanisa Katoliki ambayo Bwana aliitoa, Mitume waliihubiri na mababu waliitunza”.
Hivyo alitetea uwepo wa Utatu “kikwelikweli” na kusisitiza kwamba Neno hakuumbwa bali alizaliwa na kuwa na umungu uleule wa Baba. Mwana ana utimilifu wa umungu na ni Mungu kamili. Baba na Mwana wana hali ileile ya milele. Hiyo ni muhimu kuhusu ukombozi, kwa sababu tusingeweza kuokolewa bila Mungu kujifanya mtu. Ndiyo sababu Bikira Maria anaweza kuitwa Mama wa Mungu. Roho Mtakatifu hawezi kuwa kiumbe ndani ya Utatu, bali ni Mungu yule yule.
Orodha ya maandishi yake
[hariri | hariri chanzo]- Dhidi ya Wapagani
- Neno aliyefanyika mwili
- Kumshusha Ario
- Luka 10:22
- Waraka
- Utetezi dhidi ya Waario
- De Decretis
- De Sententia Dionysii
- Vita S. Antonii
- Ad Episcopus Aegypti et Libyae
- Apologia ad Constantium
- Apologia de Fuga sua
- Historia Arianorum
- Hotuba 4 dhidi ya Waario
- De Synodis
- Tomus ad Antiochenos
- Ad Afros Epistola Synodica
- Historia Acephala
- Barua
Tazama pia
[hariri | hariri chanzo]- Watakatifu wa Agano la Kale
- Orodha ya Watakatifu Wakristo
- Orodha ya Watakatifu wa Afrika
- Orodha ya Watakatifu Wafransisko
- Mababu wa Kanisa
Tanbihi
[hariri | hariri chanzo]- ↑ Martyrologium Romanum: ex Decreto Sacrosancti oecumenici Concilii Vaticani II instauratum auctoritate Ioannis Pauli P.P. II promulgatum, Romae 2001, ISBN 8820972107
Vyanzo
[hariri | hariri chanzo]- Arnold, Duane W.-H., 1991 The Early Episcopal Career of Athanasius of Alexandria
- Alexander of Alexandria "Catholic Epistle", The Ecole Initiative, http://ecole.evansville.edu/arians/alex1.htm Archived 16 Desemba 2007 at the Wayback Machine.
- Arius, “Arius’ letter to Eusebius of Nicomedia” from Theodoret’s, Ecclesiastical History, ser. 2, vol. 3, 41, The Ecole Initiative, http://ecole.evansville.edu/arians/arius1.htm Archived 16 Desemba 2007 at the Wayback Machine.
- Arius, Heresy and Tradition; Rowan Williams, 1987, SCM Press, ISBN 0-334-02850-7.
- Attwater, Donald and Catherine Rachel John. The Penguin Dictionary of Saints. 3rd edition. New York: Penguin Books, 1993. ISBN 0-14-051312-4.
- Barnes, Timothy D., Athanasius and Constantius: Theology and Politics in the Constantinian Empire (Cambridge, Mass: Harvard University Press, 1993).
- Barnes, Timothy D., Constantine and Eusebius (Cambridge Mass: Harvard University Press, 1981)
- Brakke, David, 1995. Athanasius and the Politics of Asceticism
- Clifford, Cornelius, 1930, Catholic Encyclipedia, Volume 2, "Athanasius", Pgs: 35-40
- Chadwick, Henry, “Faith and Order at the Council of Nicaea”, Harvard Theological Review LIII (Cambridge Mass: 1960), 171-195.
- Endsjø, Dag Øistein 2008. Primordial landscapes, incorruptible bodies. Desert asceticism and the Christian appropriation of Greek ideas on geography, bodies, and immortality. New York: Peter Lang 2008
- Ernest, James D., The Bible in Athanasius of Alexandria (Leiden: Brill, 2004).
- Haas, Christopher “The Arians of Alexandria”, Vigiliae Christianae Vol. 47, no. 3 (1993), 234-245.
- Hanson, R.P.C., The Search for the Christian Doctrine of God: The Arian Controversy, 318-381 (T.&T. Clark 1988)
- Kannengiesser, Charles, “Alexander and Arius of Alexandria: The last Ante-Nicene theologians”, Miscelanea En Homenaje Al P. Antonio Orbe Compostellanum Vol. XXXV, no. 1-2. (Santiago de Compostela, 1990), 391-403.
- Kannengiesser, Charles “Athanasius of Alexandria vs. Arius: The Alexandrian Crisis”, in The Roots of Egyptian Christianity (Studies in Antiquity and Christianity), ed. Birger A. Pearson and James E. Goehring (1986), 204-215.
- Ng, Nathan K. K., 2001 The Spirituality of Athanasius
- Rubenstein, Richard E., When Jesus Became God: The Epic Fight over Christ’s Divinity in the Last Days of Rome (New York: Harcourt Brace & Company, 1999).
- Williams, Rowan: "Arius, Heresy and Tradition": (London: Darton, Longman and Todd, 1987).
Viungo vya nje
[hariri | hariri chanzo]- Maandishi yake yote katika Patrologia Graeca ya Migne, pamoja na faharasa na tafsiri mbalimbali (EN, GR, LA, ES, RU)
- Saint Athanasius by F. A. Forbes
- The Coptic Synexarion commemorating the departure of St. Athanasius the Apostolic (7 Bashans, 89 A.M.)
- Athanasius Bibliography from University of Erlangen (German)
- Archibald Robinson, Athanasius: Select Letters and Works (Edinburgh 1885)
- The so-called Athanasian Creed (not written by Athanasius, see Athanasian Creed above)
- Athanasius Select Resources, Bilingual Anthology (in Greek original and English)
- Two audio lectures about Athanasius on the Deity of Christ Archived 2 Mei 2014 at the Wayback Machine., Dr N Needham
- Concorida Cyclopedia: Athanasius Archived 16 Julai 2011 at the Wayback Machine.
- Christian Cyclopedia: Athanasius
- Opera Omnia by Migne, Patrologia Graeca with analytical indexes
- St Athanasius the Great the Archbishop of Alexandria Orthodox icon and synaxarion
- English Key to Athanasius Werke
- The Writings of Athanasius in Chronological Order