Benito Mussolini

(Elekezwa kutoka Mussolini)

Benito Amilcare Andrea Mussolini (Dovia di Predappio, Romagna, 29 Julai 1883 - Dongo, Lombardia, 28 Aprili 1945) alitawala Italia kidikteta kati ya miaka 1922 na 1943.

Mussolini pamoja na Hitler mwaka 1940 wakitembelea Yugoslavia.

Mwanasiasa wa Kisoshialisti

hariri

Alisoma ualimu lakini alijiunga na siasa na kuwa mwanachama wa chama cha kijamaa (soshalisti) cha Italia. Akawa mhariri mkuu wa gazeti la chama.

Wakati wa Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia alidai ya kwamba Italia ijiunge na vita dhidi ya Ujerumani akafukuzwa katika chama kilichopinga vita. Mussolini akawa mwanajeshi.

Mwanzo wa ufashisti

hariri

Baada ya vita akatunga itikadi yake ya "ufashisti" akaunda harakati ya "Fasci di Combattimento" (Maungano ya mapambano). Wafuasi wake mara nyingi waliwahi kuwa wanajeshi wasioridhika na matokeo ya vita na siasa ya nchi. Mussolini aliwavalisha sare nyeusi na kuwapanga katika vikosi kwa utaratibu wa kijeshi. Idadi yao iliendelea kukua haraka hadi kufikia 200,000 mwaka 1922. "Mashati meusi" walishambulia Wakomunisti na Wasoshalisti na kuvunja migomo ya wafanyakazi wakipokea pesa kutoka kwa wenye viwanda au mashamba makubwa.

Kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 1921 Wafashisti walipata wabunge 34. Mussolini alibadilisha "fasci" kuwa chama cha kifashisti cha kitaifa (PNF). Wakati huohuo "mashati meusi" waliendela kupigana na wafanyakazi na Wasoshalisti kwenye barabara za Italia.

Kiongozi wa serikali

hariri

Hali ya vurugu ilisababisha kuanguka au kujiuzulu kwa serikali kadhaa. Mfalme Vittorio Emanuele III aliogopa vita vya wenyewe kwa wenyewe akampatia Mussolini wito wa kuanzisha serikali mpya. Hivyo tarehe 31 Oktoba 1922 Mussolini alikuwa waziri mkuu wa Italia na kiongozi wa serikali.

Tangu mwaka 1924 aliimarisha utawala wake. Kwa sheria maalumu alibadilisha utaratibu wa uchaguzi akajipatia wabunge wengi. Sheria zilizofuata zilipiga marufuku vyama vya upinzani. Wanahabari wote walipaswa kuwa wanachama wa chama cha kifashisti. Kufikia mwaka 1928 udikteta wa chama kimoja ulikuwa umesimama imara.

Siasa ya nje

hariri

Dikteta Mjerumani Adolf Hitler alikuwa amevutwa na siasa ya Mussolini akamwiga katika mengi. Lakini Mussolini hakumpenda Hitler, hasa itikadi yake ya kimbari. Alikuwa na wasiwasi kuhusu mipango ya Hitler dhidi ya Austria. Mwaka 1934 alituma wanajeshi mpakani mwa Austria akiogopa uvamizi wa Wajerumani katika nchi ya jirani.

Katika siasa ya nje Mussolini alikuwa na ndoto ya kujenga upya Dola la Roma la Kale. Mwaka 1935 alishambulia Ethiopia akitaka kujipatia koloni jipya na pia kulipiza kisasi cha ushindi wa Ethiopia dhidi ya Italia katika mapigano ya Adowa ya mwaka 1896. Italia ikafukuzwa katika Shirikisho la Madola lakini ilifaulu kutawala Ethiopia yote kwa kutumia hata silaha za kikemikali.

Katika Vita ya wenyewe kwa wenyewe ya Hispania tangu mwaka 1936 Mussolini alichukua upande wa jenerali Francisco Franco. Kufukuzwa katika Shirikisho la Madola na msaada kwa Franco kulisababisha hali ya kuwa karibu zaidi na Hitler. Tarehe 25 Oktoba 1936 Mussolini na Hitler walitia sahihi mkataba wa ushirikiano kati ya Italia na Ujerumani.

 
Benito Mussolini, hawara wake Claretta Petacci na wengineo wakionyeshwa hadhara ya watu baada ya kuuawa.

Vita Kuu ya Pili ya Dunia

hariri

Albania

hariri

Katika Aprili 1939 - kabla ya mwanzo wa Vita Kuu - Italia ilivamia Albania. Jeshi la Italia lilipata matatizo makubwa kushinda nchi hii ndogo. Hivyo Mussolini alipomwona Hitler kushambulia Poland tarehe 1 Septemba 1939, mwanzoni alitulia.

Ufaransa

hariri

Alikaa kimya pia Hitler alipovamia Ufaransa. Mwishoni tu, siku chache kabla ya ushindi wa Ujerumani kukamilika, Mussolini aliamua kuingia katika vita akateka sehemu ndogo ya Ufaransa kusini.

Ugiriki

hariri

Tarehe 28 Oktoba 1940 Mussolini aliamrisha jeshi lake kushambulia Ugiriki. Lakini Wagiriki walijitetea kwa nguvu Waingereza wakawasaidia. Jeshi la Wagiriki liliingia katika Albania. Hitler alipaswa kuingilia kati na kutuma wanajeshi Wajerumani Ugiriki waliofaulu kuwashinda Wagiriki na Waingereza nchini.

Afrika

hariri

Mussolini alikuwa na matumaini ya kwamba ingekuwa rahisi kuvamia na kuteka makoloni ya Uingereza katika Afrika. Alipanga kuwashambulia Waingereza kutoka makoloni ya Italia ya Libya, Ethiopia na Somalia akilenga Misri, Somalia ya Kiingereza na Kenya. Lakini mipango hii pia ilishindikana.

Mwisho

hariri

Wakati huohuo Uingereza ilizamisha manowari nyingi za Italia. Mwaka 1943 Waingereza na Wamarekani -waliowahi kuteka Afrika ya Kaskazini- walivamia Italia ya kusini.

Mussolini aliangushwa na halmashauri ya chama chake pamoja na mfalme akatupwa katika jela. Wajerumani walimwokoa gerezani lakini hakuweza kutawala Italia tena. Alikuwa na eneo dogo katika Italia ya Kaskazini.

Katika siku za mwisho wa vita kuu Mussolini alijaribu kujiokoa mbele ya jeshi la Wamarekani waliokaribia kwa kukimbilia Uswisi. Tarehe 27 Aprili 1945 Mussolini pamoja na wasaidizi wake na mpenzi wake Clara Petacci walikamatwa na wanamgambo Waitalia Wakomunisti waliomwua siku iliyofuata, tarehe 28 Aprili.