Karl Friedrich Benz

(Elekezwa kutoka Karl Benz)


Karl Friedrich Benz alizaliwa tar. 25 Novemba 1844 akiitwa Karl Friedrich Michael Vaillant huko Mühlburg / Karlsruhe Ujerumani wa Kusini Magharibi. Baada ya kumzaa mamake Josephine Vaillant akaolewa na babake Johann Georg Benz. Hivyo akaitwa Karl Friedrich Michael Benz lakini baadaye akajiita Carl Friedrich Benz.

Alikuwa mhandisi Mjerumani mwenye sifa ya kuwa alitengeza motokaa ya kwanza au gari la kwanza lililotumia nguvu ya nishati ya petroli.

Mwaka 1864 alichukua digri ya uhandisi, mw. 1871 alianzisha kampuni yake ya kwanza. Hapo alitengeneza injini ya petroli ya mapigo mawili mwaka 1878/79 aliyoendeleza kuwa injini ya mapigo manne. Benz hakuwa mhandisi wa kwanza kutengeneza injini za aina hii, Mjerumani mwenzake Nikolaus Agosti Otto aliwahi kuchukua hataza ya injini ya mapigo manne mwa. 1876. Injini za aina hii zilifanya kazi viwandani vikiendesha mashine mbalimbali.

1886 Benz alikuwa mtu wa kwanza aliyeweka injini ya petroli kwa gari. Gari lake la kwanza lilikuwa na magurudumu matatu yenye nguvu-farasi 0.8. Mke wake Bertha Benz alifanya safari kubwa ya kwanza kwa gari hili kwa umbali wa km 89 kutoka Mannheim kwenda Pforzheim (yote Ujerumani wa Kusini Magharibi). Alipoishia petroli alipaswa kuinunua katika duka ya madawa kwani hapakuwapo na kituo cha petroli bado.

Benz aliendelea kutengeneza gari lenye magurudumu manne. Kwa jina la "Velo" lilikuwa motokaa ya kwanza iliyotengenezwa kwa wingi duniani.

Benz aliona kupanuka kwa biashara yake watoto wake wakiendelea kuendesha makampuni yake. Mwaka 1926 kampuni ya Benz iliunganishwa na kampuni ya Gottlieb Daimler kwa jina la "Daimler-Benz".

Karl Benz aliaga dunia tar. 4 Aprili 1929.

Viungo vya Nje

hariri