Satyagraha
Satyagraha ni falsafa na zoezi la siasa ya upinzani bila ya kufanya fujo iliyobuniwa na Mohandas Karamchand Gandhi (aliyejulikana pia kama "Mahatma", yaani "Roho kubwa"). Mtu anayefuata maadili ya satyagraha huitwa mwanasatyagrahi.
Gandhi, ambaye aliathiriwa sana na hotuba ya mlimani ya Yesu (Math 5-7), alitumia satyagraha kwa kampeni za kupigania uhuru wa Uhindi na pia wakati wa mapambano yake ya hapo awali katika nchi ya Afrika Kusini dhidi ya ubaguzi.
Nadharia ya satyagraha iliwashawishi Nelson Mandela na kabla yake Martin Luther King hasa wakati alipoongoza kampeni za harakati za haki za kiraia nchini Marekani, pamoja na harakati za haki za kijamii na harakati nyinginezo.
Maana ya neno
[hariri | hariri chanzo]Satyagraha inatokana na kuyaunganisha maneno ya Kisanskriti Satya (linalomaanisha ukweli) na "Agraha" ("kusisitiza" au "kushikilia kwa imara"). Kwa Gandhi, satyagraha ilikuwa na maana zaidi kuliko "upinzani bila ya fujo" na ikawa nguvu katika utumizi wa njia zisizo za fujo. Kwa mujibu wa maneno yake:
Ukweli (satya) kunaashiria upendo, na kuwa imara (agraha) kunasababisha, na hivyo basi kunakuwa kisawe cha nguvu. Hivyo basi mimi nilianza kuzipa harakati za Kihindi jina Satyagraha, hivyo ni kusema, Nguvu ambayo inatokana na Ukweli na Upendo au isiyo na fujo, nikaacha kuyatumia maneno "upinzani usiokuwa na fujo", kufanya uhusiano na nadharia hiyo, kiasi kwamba hata katika maandishi katika lugha ya Kiingereza mara nyingi sisi tuliliepuka na kutumia badala yake neno "satyagraha ".... ”....[1]
Katika barua aliyoandika kwa P. K. Rao, Watumishi wa Jamii ya Kihindi ya tarehe 10 Septemba 1935, iliyonukuliwa katika kitabu cha Louis Fischers, Maisha ya Mahatma Gandhi, Sehemu I, Sura 11, uk. 87-88, Gandhi anakana kuwa wazo lake la Kutotii kwa Raia lilitokana na maandiko ya Thoreau.
"Taarifa kwamba mimi nilikuwa nimeliazima wazo langu la Kutotii kwa Raia kuelezea mapambano yetu kwa wasomaji wa Kiingereza. Lakini nilipata kwamba hata "Kutotii kwa Raia" kulishindwa kuipa maana kamili ya mapambano. Kwa hiyo, mimi nilibuni maneno "Mapinzani ya Raia."
Gandhi alielezea Mapinzani ya Raia ifuatavyo:
Mimi pia nimeipa jina pendo-nguvu au nafsi-nguvu. Katika kuitumia satyagraha, mimi niligundua katika hatua za mwanzo kwamba harakati za kuutafuta ukweli haikukubali vurugu ifanywe dhidi ya mpinzani bali kwamba ni lazima yeye aondolewe kutoka makosa yake kupitia uvumilivu na huruma. Kwani linaloonekana kuwa ni la kweli kwa mmoja huenda likaonekana kuwa kosa kwa mwingine. Na maana ya uvumilivu ni mateso ya mtu nafsi yake. Kwa hiyo mafundisho yamekuja kumaanisha kubainika wazi kwa ukweli, si kwa kumtesa mpinzani, bali kwa kujisababishia mateso mwenyewe. [2]
Ikitofautishwa na “upinzani bila fujo”
[hariri | hariri chanzo]Gandhi alitofautisha satyagraha na upinzani bila fujo katika barua ifuatayo:
"Nimetofautisha upinzani bila fujo jinsi inavyoeleweka na kutumika katika nchi za Magharibi na satyagraha kabla ya kuyabuni mafundisho ya satyagraha kwa kiwango kamili cha kimantiki na cha kiroho. Kuwa tulivu ina maana ya karibu na kutokuwa na fujo. Mimi mara nyingi niliyatumia maneno "upinzani bila fujo" na "satyagraha" kama maneno yenye maana sawa: lakini kadri mafundisho ya satyagraha yalivyoendelea, maneno "upinzani bila fujo" yanasita kulenga maana sawa, kwani upinzani bila fujo umekubali kufanya ghasia haswa katika mfano wa wapigaji kura na imekubalika ulimwenguni kote kuwa silaha ya wanyonge. Aidha, upinzani bila fujo hakuitaji kushikilia kikamilifu ukweli kila wakati. Kwa hivyo ni tofauti na satyagraha katika maswala matatu muhimu: Satyagraha ni silaha ya wenye nguvu; inakubali kutotumia fujo katika hali yoyote ile; na milele inasisitiza ukweli utumike. Nafikiri sasa nimeifanya tofauti iwe wazi kabisa. "[3]
Nadharia ya Satyagraha
[hariri | hariri chanzo]Mafanikio ya wazi
[hariri | hariri chanzo]Katika migogoro ya kale inayotumia na isiyotumia fujo, lengo ni kumshinda mpinzani au kuyafanya anayolenga yawe magumu kupata, au kuyatimiza malengo ya kibinafsi licha ya juhudi za mpinzani kuyapinga. Katika satyagraha, kwa kutofautisha, haya sio malengo. "Lengo lake Mwanasatyagrahi's ni kumbadili, si kumdhulumu, mtendamabaya." [4] Mafanikio hufafanuliwa kama kushirikiana na mpinzani kupata matokeo ambao mpinzani anayapinga bila kujua. Lazima mpinzani abadilishwe fikra, angalau aache kufanya iwe vigumu kupata la haki linalowaniwa, ili ushirikiano huu uweze kufanyika.
Mbinu na matokeo
[hariri | hariri chanzo]Nadharia ya satyagraha inazitazama mbinu na matokeo kama dhana tusizoweza kutenga. Njia inayotumika kupata matokeo fulani zimefungwa ndani ya na kushikana na matokeo hayo. Kwa hiyo, kuna utata katika kujaribu kuitumia njia za kudhulumu kuipata haki au kujaribu kuitumia fujo kuipata amani. Gandhi alivyoandika: "Wao husema, 'mbinu ni, baada ya yote, mbinu tu'. Naweza kusema, 'mbinu ni, baada ya yote, kila kitu'. Kama ilivyo mbinu basi ulivyo mwisho ... "[5]
Gandhi aliutumia mfano kulifafanua wazo hili:
Nikitaka kukunyima saa yako, bila shaka itanibidi niipiganie; nikitaka kuinunua saa yako, itanibidi nikulipe; na kama nataka zawadi, itabidi nikusihi unipe; na, kulingana na mbinu nitakayoitumia, saa hiyo ni mali ya wizi, mali yangu mwenyewe, au mchango. [6]
Gandhi alilikataa wazo kwamba udhalimu unafaa, au hata ungeweza, kupingwa "kwa njia yoyote ile" - ikiwa unatumia mbinu za fujo, za kudhulumu, mbinu zisizokuwa za haki, yoyote utakayoyapata mwishowe lazima yatazidisha udhalimu huo. Kwa wale ambao walihubiri fujo huku wakiwaita waliochukua hatua zisizokuwa za fujo woga, yeye alijibu: "Naamini kuwa, ambapo kuna uchaguzi tu kati ya woga na fujo, ningeshauri fujo itumike....Kwangu heri Uhindi ianze kuzitumia silaha ili kulinda heshima yake kuliko, kwa namna ya woga, iwe au ibaki shahidi asiyeweza kujisaidia inavyokosewa heshima...Lakini naamini kwamba kutotumia fujo kumeishinda fujo kwa mbali, msamaha ni ishara zaidi ya uume kuliko adhabu." [7]
Satyagraha ikitofautishwa na Duragraha
[hariri | hariri chanzo]Kiini cha Satyagraha ni kwamba inalenga kuondoa dhuluma bila kuwadhuru wanaodhulumu, kinyume na upinzani wa fujo, ambayo inalenga kusababisha madhara kwa mdhulumu. Mwanasatyagrahi kwa hiyo halengi kuumaliza au kuuharibu uhusiano na mdhulumu, bali analenga kuubadilisha au "kuusafisha" kwenda nyanja cha juu. Maneno ya heshima yanayotumika wakati mwingine kwa Satyagraha ni kwamba ni "kimya nguvu" au "roho nguvu" (maneno ambayo pia yametumiwa na Martin Luther King Jr wakati wa hotuba yake maarufu ya "Nina Ndoto"). Inampa mtu binafsi silaha ya maadili wala si nguvu za kimwili. Satyagraha pia inafahamika kama "nguvu za ulimwenguni kote," kwani kwa kiini "haitofautishi kati ya jamaa na wageni, vijana na wazee, mwanamume na mwanamke, rafiki na adui." [8]
Gandhi aliitofautisha satyagraha (kuushikilia ukweli) na "duragraha" (kuishikilia nguvu), kama katika mfano wa maandamano yanayolenga kuwasumbua kuliko kuwaelimisha wapinzani. Yeye aliandika: "Lazima kusiwe na pupa, kusiwe na unyama, kusiwe na ukosefu wa heshima, kusiwe na kulazimisha kwingi. Ikiwa tunataka kujenga roho ya kweli ya demokrasia, hatuwezi kumudu kutowavumilia wengine. Kutovumilia kunasaliti ukosefu wa imani katika harakati ambayo mtu anapigania. "[9]
Kutotii kwa raia na kutoshirikiana kama inavyofanywa katika Satyagraha kumebuniwa kutoka "sheria ya mateso", [10] fundisho kwamba uvumilivu matesoni ni mbinu ya kupata matokeo fulani. Matokeo haya kwa kawaida yanadokeza kuinuliwa au kuendelea kwa mtu binafsi au jamii kimaadili. Kwa hiyo, kutoshirikiana katika Satyagraha kwa kweli ni njia ya kupata ushirikiano wa mpinzani huku ukweli na haki zikisisitizwa.
Satyagraha katika migogoro mikubwa
[hariri | hariri chanzo]
Wakati wa kuitumia satyagraha katika migogoro mikubwa ya kisiasa inayohusu kutotii kwa raia, Gandhi aliamini kwamba lazima masatyagrahi wapitie mafunzo ili kuhakikisha nidhamu ipo. Aliandika kwamba "Ni wakati tu ambapo watu wamethibitisha mazoea ya utii kwa kutii sheria nyingi za Nchi ndivyo wanapata haki ya Kutotii kwa Raia." [11]
Basi akaifanya sehemu ya nidhamu ya masatyagrahi iwe:
- fahamu zile sheria nyingine za Nchi na uzitii kwa hiari
- vumilia sheria hizi, hata zinapokuwa ngumu kutekeleza
- kuwa tayari kupitia mateso, kupoteza mali, na kuvumilia mateso ambayo huenda yakatendewa familia na marafiki [11]
Kutii huku kusiwe kwa dharau, yafaa kusiwe kwa kawaida:
... Mtu mwaminifu na wa kuheshimika hataanza kuiba ghafla sheria dhidi ya kuiba iwepo au la, lakini huyu mtu hatahisi aibu yoyote kwa kutoifuata sheria ya kuzibeba taa baiskelini baada ya giza.... Lakini ataifuata sheria yoyote ya lazima ya namna hii, mradi tu aiepuke shida ya kukabiliwa na mashtaka ya uvunjaji wa sheria hiyo. Kutii kwa aina hii si, hata hivyo, kutii kunaotokana na nia na kwa mara moja kunaotakiwa na Satyagrahi. [12]
Kanuni kwa Wanasatyagrahi
[hariri | hariri chanzo]Gandhi alinuia satyagraha iwe si mbinu tu ya kutumika katika mapambano ya kisiasa, lakini iwe kama solventa ulimwenguni kote dhidi ya dhuluma na madhara. Alihisi kuwa ingeweza kutumika kwa mapambano makubwa ya kisiasa na mapambano ya moja-kwa-moja kati ya watu na kuwa ilipaswa kufunzwa kwa kila mtu. [13]
Alianzisha Sabarmati Ashram kufunza satyagraha. Aliwaomba wanasatyagrahi kufuata kanuni zifuatazo (Yamas zinazoelezewa katika Yoga Sutra): [14]
- Kupinga fujo (ahimsa)
- Kweli - hili ni pamoja na uaminifu, lakini huzidi na kumaanisha kuishi kikamilifu, pamoja, na katika ibada na yale ambayo ni ya kweli
- Kutoiba
- Utakatifu (brahmacharya) - hili ni pamoja na usafi wa kujuana kimwili, na pia kupunguza tamaa zingine za kimwili kwa bidii ya kimsingi ambayo ni kuutafuta ukweli
- Kutomiliki (si sawa na umaskini)
- Kazi-mwili au Kazi-mkate
- Udhibiti wa mdomo
- Kutokuwa na woga
- Heshima sawa kwa dini zote
- Mikakati ya kiuchumi kama vile migomo (swadeshi)
- Uhuru kutoka hali ya kutoguzika
Wakati mwingine, aliziorodhesha kanuni saba ambazo ni "muhimu kwa kila Mwanasatyagrahi katika nchi ya Uhindi": [15]
- lazima awe na imani katika Mungu aliye hai
- lazima aamini ukweli na aamini mtazamo wa kutofanya fujo na awe na imani katika wema wa kindani wa hali ya kibinadamu ambayo yeye anatarajia kuibua kupitia mateso katika juhudi za satyagraha
- lazima awe anaongoza maisha mema, na awe tayari kufa au kupoteza mali yake yote
- lazima awe na tabia ya kulivaa vazi la 'khadi na kulishona
- lazima ajiepushe na pombe na vileo vingine.
- lazima atimize kwa hiari kanuni zote za nidhamu zinazotolewa
- lazima atii sheria za jela isipokuwa zinapoundwa haswa kwa minajili ya kumkosea heshima
Kanuni za Kampeni za Satyagraha
[hariri | hariri chanzo]Gandhi alipendekeza mfululizo wa sheria kwa Wanasatyagrahi kufuata katika kampeni ya upinzani: [8]
- usiwe na hasira
- teseka kutokana na hasira ya mpinzani
- usilipize kisasi kamwe kwa mashambulizi au adhabu; lakini usikubali, kwa sababu ya hofu ya adhabu au kushambuliwa, amri iliyotolewa kwa hasira
- kubali kwa hiari kukamatwa au kuchukuliwa kwa mali yako
- ikiwa wewe ni mdhamini wa mali, linda mali hayo kwa maisha yako (bila fujo) yasinyakuliwe
- usilaani wala usiape
- usimtusi mpinzani
- usiionyeshe heshima wala usiitukane bendera ya mpinzani wako au viongozi wa mpinzani wako.
- ikiwa mtu yeyote atajaribu kumtusi au kumshambulia mpinzani wako, mtetee mpinzani wako (bila fujo) hata kwa kuyahatarisha maisha yako
- kama mfungwa, kuwa na tabia nzuri gerezani na utii kanuni za gereza (isipokuwa zozote ambazo ni kinyume na heshima uliyonayo)
- kama mfungwa, usiombe kufanyiwa mapendeleo maalum
- kama mfungwa, usifunge ukinuia kupata mazuri ambayo ikiwa ungenyimwa, haungepata majeraha yoyote kwa heshima yako ya kibinafsi
- tii kwa furaha amri za viongozi wa hatua za kutotii kwa raia.
- usichague miongoni mwa amri unazozitii; ikiwa unaona hatua nzima haifai, kata uhusiano wako na hatua hiyo kabisa
- usifanye kushiriki kwako kutegemee ndugu zako kuwatunza wanaokutegemea wakati wewe unajishughulisha na kampeni au wakati unapokuwa gerezani; usitarajie wao kukupa msaada wa aina hiyo.
- usiwe chanzo ya kuibuka kwa ugomvi katika jumuiya
- Usichague pande katika ugomvi kama huo, lakini saidia tu upande ambao unaonekana kuwa wa haki; katika vita kati ya dini tofauti, toa maisha yako kulinda (bila fujo) wale walio katika hatari katika upinzani
- epuka hafla zinazoweza kuzua ugomvi katika jumuiya
- usijiusishe na maandamano ambayo huenda yakaumiza imani ya kidini ya jamii yoyote
Satyagraha na harakati za haki za kiraia nchini Marekani
[hariri | hariri chanzo]Nadharia ya Satyagraha pia ilimshawishi Martin Luther King wakati wa kampeni alizoongoza wakati wa harakati za haki za kiraia nchini Marekani:
Kama watu wengine wengi, mimi nilikuwa nimesikia kumhusu Gandhi, lakini kamwe sikuwa nimewahi kuvisoma vitabu vyake kwa uzito unaostahili. Kadri nilivyovisoma ndivyo nilivyoguzwa kwa undani na kampeni zake za upinzani bila fujo. Mimi niliguzwa hasa na maandamano yake ya chumvi kwenda baharini na kufunga kwake wa mara kwa mara. Dhana yote ya Satyagraha (Satya ni ukweli ambayo ni sawiaa na upendo, na agraha ni nguvu; Satyagraha, kwa hiyo, inamaanisha nguvu-pendo au pendo-nguvu) ilikuwa muhimu sana kwangu. Kadiri nilivyoingia ndani zaidi katika falsafa ya Gandhi, ndivyo shaka yangu kuhusu nguvu za upendo ilipopotea polepole, na nilikuja kuona kwa mara ya kwanza nguvu za falsafa ile katika mageuzi ya kijamii... Ilikuwa katika kusisitiza kwa Gandhi kwa upendo na kutofanya fujo ambapo niligundua njia ya mageuzi ya kijamii niliyokuwa nikiitafuta. [16]
Satyagraha na mauaji ya kimbari ya Wayahudi
[hariri | hariri chanzo]Katika mtazamo wa Wanaksi kuwatesa Wayahudi nchini Ujerumani, Gandhi alipendekeza Satyagraha kama njia ya kupambana na uonevu na mauaji ya halaiki ya watu, inayosema:
Ningalikuwa Muyahudi na ningalizaliwa nchini Ujerumani na kuwa na kazi pale, ningalidai Ujerumani kama nyumbani hata kama Mjerumani mrefu zaidi mwenye nguvu angeweza kudai, na kumpa changamoto anipige risasi au anitupe gerezani; Mimi ningekataa kukubali kufukuzwa au kubaguliwa. Na kwa kufanya hayo mimi sipaswi kuwasubiri Wayahudi wenzangu kujiunga nami katika upinzani wa kiraia, bali ningeamini kwamba mwishowe wengine hawangekuwa na budi kuufuata mfano wangu. Kama Myahudi mmoja au Wayahudi wote wangalikubali tiba iliyopewa hapa, yeye au wao hawangalikuwa katika hali mbaya zaidi kuliko ile waliyomo kwa sasa. Na kuteseka kwa hiari kungewapa nguvu na furaha ya ndani[...] unyanyasaji wa kimakusudi kwa Hitler kunaweza hata kusababisha mauaji ya kijumla ya Wayahudi kwa njia ya jibu lake la kwanza kwa azimio la uadui wa aina hiyo. Lakini ikiwa akili ya Kiyahudi ingeweza kutayarishwa kupitia mateso ya hiari, hata mauaji ninayowaza yangegeuzwa yawe siku ya shukrani na furaha kwamba Bwana alitenda kwa mikono ukombozi wa tabaka fulani hata mikononi mwa mnyanyasaji. Kwa wachamungu, kifo hakitishi. [17]
Gandhi alilaumiwa vikali kwa kauli hizi akajibu katika makala mengine kwa jina "Majibu kwa Baadhi ya Maswali" ambapo aliandika:
Marafiki wamenitumia vipandikizi vya magazeti mawili vinavyokosoa ombi langu kwa Wayahudi. Wakosoaji hao wawili wanaamini kwamba katika kuwasilisha kutofanya fujo kwa Wayahudi kama dawa dhidi ya makosa waliyofanyiwa, sijapendekeza chochote kipya... Kile nilichoomba ni kuikana fujo ya roho na baada ya hapo mazoea ya kuitumia nguvu inayotokana na kuukana kule kukubwa." [18]
Aidha, akitazamia uwezekano wa India kushambuliwa na Japan wakati wa Vita vya pili vya Dunia, Gandhi alipendekeza satyagraha kama ulinzi:
... Yafaa pawe na kutoshirikiana bila fujo na bila doa, na ikiwa nchi yote ya Uhindi iliitikia na kwa umoja ikapena kutoshiriki kwake, mimi napaswa kuonyesha kuwa, bila kumwaga tone moja la damu, silaha za Kijapani - au mchanganyiko wa silaha zozote - unaweza kusafishwa. Hilo linahusu uamuzi wa Uhindi wa kutopeana robo au nukta yoyote na kuwa tayari kukabiliana na hatari ya kuyapoteza mamilioni kadhaa ya maisha. Lakini ningefikiria gharama hiyo kuwa nafuu sana na ushindi uliopatikana kwa gharama hiyo kuwa tukufu. Ni kweli kuwa India huenda ikawa haijajitayarisha kuilipa bei hiyo. Natumai sio kweli, lakini gharama kama hiyo lazima ilipwe na nchi yoyote inayotaka kuurejesha uhuru wake. Baada ya yote, sadaka iliyotolewa na Warusi na Wachina ni kubwa, na wako tayari kuyahatarisha yote. Hayo pia yanawezwa kusemwa kuhusu nchi nyingine pia, ziwe zinazoshambulia au zinazolinda. Gharama ni kubwa sana. Hiyo, katika mbinu ya kutofanya fujo nauliza Uhindi isiyahatarishe zaidi kuliko jinsi nchi nyingine zinavyohatarisha, na ambayo Uhindi ingebidi kuyahatarisha hata kama ingetumia upinzani wa silaha. [19]
Mchanganyiko wa falsafa ya Gandhi ya kuikana fujo pamoja na mazoea ya kuyakubali mateso pia ilikubalika na wataalam wa Kiyahudi. Mwanaelimunafsia wa tabia zisizo za kawaida za binadamu Victor Frankl na mwanaelimunafsia wa tabia za kawaida za binadamu Bruno Bettelheim, wote waathiriwa wa mauaji ya halaiki ya Wayahudi, walithibitisha uzoefu wa Gandhi kwamba watu ambao hawakubali kimya tu wala kulipiza kisasi wanapofanyiwa fujo hupata ndani yao hisia mpya ya nguvu, hadhi, na ujasiri. [1] Mbinu ya Gandhi imelinganishwa na ile ya Frankl. [2]
Maandishi ya Chini
[hariri | hariri chanzo]- ↑ Satyagraha in South Africa, 1926 from Johnson, p. 73.
- ↑ Gandhi, M.K. Statement to Disorders Inquiry Committee 5 Januari 1920 (The Collected Works of Mahatma Gandhi vol. 19, p. 206)
- ↑ Gandhi, M.K. “Letter to Mr. ——” 25 Januari 1920 (The Collected Works of Mahatma Gandhi vol. 19, p. 350)
- ↑ Gandhi, M.K. “Requisite Qualifications” Harijan 25 Machi 1939
- ↑ R. K. Prabhu & U. R. Rao, editors; from section “The Gospel Of Sarvodaya, of the book The Mind of Mahatma Gandhi Archived 20 Desemba 2010 at the Wayback Machine., Ahemadabad, India, Revised Edition, 1967.
- ↑ Gandhi, M.K. “Brute Force”, Chapter XVI of Hind Swaraj, 1909 (The Collected Works of Mahatma Gandhi vol. 10, p. 287)
- ↑ R. K. Prabhu & U. R. Rao, editors; from section “Between Cowardice and Violence,” of the book The Mind of Mahatma Gandhi Archived 20 Desemba 2010 at the Wayback Machine., Ahemadabad, India, Revised Edition, 1967.
- ↑ 8.0 8.1 Gandhi, M.K. “Some Rules of Satyagraha” Young India (Navajivan) 23 Februari 1930 (The Collected Works of Mahatma Gandhi vol. 48, p. 340)
- ↑ R. K. Prabhu & U. R. Rao, editors; from section “Power of Satyagraha,” of the book The Mind of Mahatma Gandhi Archived 20 Desemba 2010 at the Wayback Machine., Ahemadabad, India, Revised Edition, 1967.
- ↑ Gandhi, M.K. “The Law of Suffering” Young India 16 Juni 1920
- ↑ 11.0 11.1 Gandhi, M.K. “Pre-requisites for Satyagraha” Young India 1 Agosti 1925
- ↑ Gandhi, M.K. “A Himalayan Miscalculation” in The Story of My Experiments with Truth Chapter 33
- ↑ Gandhi, M.K. “The Theory and Practice of Satyagraha” Indian Opinion 1914
- ↑ Gandhi, M.K. Non-violent Resistance (Satyagraha) (1961) p. 37
- ↑ Gandhi, M.K. “Qualifications for Satyagraha” Young India 8 Agosti 1929
- ↑ King, Jr., Martin Luther (1998). Carson, Clayborne (mhr.). The Autobiography of Martin Luther King, Jr. ku. 23–24. ISBN 0446524123.
- ↑ Gandhi, M.K. “The Jews” Harijan 26 Novemba 1938 (The Collected Works of Mahatma Gandhi vol. 74, p. 240)
- ↑ Gandhi, M.K. “Some Questions Answered” Harijan 17 Desemba 1938 (The Collected Works of Mahatma Gandhi vol. 74, p. 297-8)
- ↑ Gandhi, M.K. “Non-violent Non-cooperation” Harijan 24 Mei 1942, p. 167 (The Collected Works of Mahatma Gandhi vol. 82, p. 286; interview conducted 16 Mei 1942)