Kwanzaa
Kwanzaa ni sikukuu inayosherehekewa kati ya Wamarekani Weusi nchini Marekani kwa muda wa siku saba toka tarehe 26 mwezi wa disemba hadi tarehe 1 mwezi wa Januari. Sikukuu hii ilianzishwa Kalifornia na Maulana Ron Karenga tarehe 26 Diesemba mwaka 1966.
Karenga alitunga neno jipya "Kwanzaa" kutokana na neno la Kiswahili "Kwanza" inayochukuliwa kumaanisha "matunda ya kwanza". Herufi "a" iliongezwa katika neno hilo ili kulifanya neno hilo kuwa na herufi saba, sawa na idadi ya siku za kusherehekea sikukuu hii. [1]
Baadhi ya waamerika weusi huchukulia sikukuu hii kuwa na umuhimu sana kwao kama vile ilivyo Hanuka kwa Wayahudi au Krisimasi kwa Wakristo. Karenga aliagiza kutumia maneno kadhaa ya Kiswahili katika sikukuu hizi kwa kuonyesha uhusiano na utamaduni wa Afrika.
Sherehe hii imejengwa juu ya maadili ya kitamaduni ya Kiafrika na huchukuliwa kuwa ni kama aina za sherehe za makabila mbalimbali Afrika wakati wa mavuno. Maadili haya ya Kiafrika yamegawanywa katika dhana iitwayo Nguzo Saba. Kwa siku saba, kila siku huwa na nguzo yake ya kukumbuka na kuenzi. Nguzo hizo ambazo zinafahamika kwa Kiswahili ni: Umoja, Kujichagulia, Ujima, Ujamaa, Nia, Kuumba, na Imani. Nguzo saba hizi hutumiwa kama moja ya njia ya kuimarisha umoja wa kifamilia miongoni mwa jamii za Wamarekani Weusi na pia njia ya kuwakumbusha historia na utamaduni wao.
Sikukuu hii inatumia alama kadhaa ambazo nazo zinatambulika kwa lugha ya Kiswahili. Alama hizo ni:
- Mazao
- Mkeka
- Kinara
- Muhindi
- Mishumaa Saba
- Kikombe cha Umoja
- Zawadi
Kati ya shughuli zinazofanywa wakati wa sikukuu hii ni kuwasha mishumaa saba (mshumaa mmoja kila siku) na kutoa tambiko la kuenzi mababu na mabibi waliotangulia. Mishumaa hii huwa ina rangi za kijani, nyekundu na nyeusi. Mshumaa mweusi huwekwa katikati na ndio huwa wa kwanza kuwashwa. Huwashwa siku ya kwanza. Rangi nyeusi huwakilisha watu weusi, rangi nyekundu hukumbusha mapambano na masahibu yaliyowakumba walitangulia, na rangi ya kijani humaanisha utajiri wa bara la Afrika na pia matumaini mema ya watu weusi.
Tanbihi
[hariri | hariri chanzo]- ↑ Katika tovuti ya Kwanzaa hali ya Juni 2014 imeandikwa kuwa herufi ya saba iliongezeka kwa sababu katika chanzo cha sikukuu kulikuwa na watoto saba waliotaka kubeba herufi moja-moja ya neno jukwaani, na kwa sababu "kwanza" ina herufi sita pekee, waliongeza herufi moja
Viungo vya nje
[hariri | hariri chanzo]- (Kiingereza) Tovuti Rasmi ya Kwanzaa
Makala hii kuhusu mambo ya utamaduni bado ni mbegu. Je, unajua kitu kuhusu Kwanzaa kama historia yake au mahusiano yake na mada nyingine? Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. |