Liberal Democratic Party (LDP) ni chama cha kisiasa nchini Kenya. Ilikuwa na wabunge 59 baada ya uchaguzi wa Kenya wa 2002 ikiwa sehemu ya NARC yaani maungano ya kisiasa tawala katika Kenya baada ya 2002. Haikugombea bunge kwa jina lake katika uchaguzi wa 2007 bali wanachama wake walishiriki katika Orange Democratic Movement.

Kukua baada ya kupokea wanachama wa KANU 2002

hariri

LDP ilikuwa chama kidogo sana bila maana yoyote hadi 2002. Mwaka ule kulikuwa na farakano katika chama tawala cha KANU. Raila Odinga aliyewahi kujiunga katika KANU 2001 pamoja na wenzake wa chama cha NDP aliondoka tena baada ya rais Daniel arap Moi kumtangaza Uhuru Kenyatta kuwa mgombea wa KANU kwa ajili ya uchaguzi wa 2002. Wanasiasa wengine wa KANU kama vile Kalonzo Musyoka, George Saitoti na wengine waliosikitika hatua hii ya Moi walienda pamoja na Odinga wakajiita harakati ya pinde (Rainbow Movement). Kwa kusudi la kuingia katika uchaguzi walihitaji kuwa haraka na chama kilichoandikishwa. Wakaogopa kuandikisha Rainbow kwa sababu hawakuwa na uhakika kama serikali ya Moi ingewazuia au la. Hapa walijiunga wote na LDP kwa sababu ilikuwa imeandikishwa tayari.

Kuunda NARC

hariri

Punde baada ya kuingia LDP viongozi walianza majadiliano na maungano wa upinzani National Alliance of Kenya (NAK) yaliyounganisha chama cha DP chini ya Mwai Kibaki na vyama vidogo vingine kama NPK ya Charity Ngilu na FORD-Kenya ya Michael Wamalwa. NAK na LDP walipatana kugombea uchaguzi pamoja kwa jina la National Rainbow Coalition (NARC). Kibaki aliteuliwa kuwa mgombea wa urais na Odinga aliahidiwa atakuwa waziri mkuu baada ya sahihisho la Katiba.

Chama tawala

hariri

NARC ilishinda na LDP ilikuwa na wabunge wengi kati ya vyama vya NARC. Lakini Kibaki hakutekeleza azimio la pamoja katika Memorandum of Understanding kupatia LDP nusu ya mawaziri wala kuwezesha mabadiliko ya katiba ya kumpa Odinga nafasi ya waziri mkuu.

LDP iliendelea kudai mapatano yafuatwe ikakataliwa na polpole kuelekea upande wa upinzani hata kama bado ilikuwa sehemu ya serikali.

Farakano ya katiba

hariri

Mwaka 2005 Kibaki alijaribu kupitisha katiba mpya isiyopungua sana madaraka yake. Hapa sehemu kubwa ya LDP pamoja na KANU wakiungana kwa harakati ya machungwa (ODM) walipinga pendekezo la katiba katika kura maalumu ya wananchi na pendekezo likakataliwa na wananchi.

Kibaki alijibu kwa kufuta serikali akiwaachisha mawaziri wote. Serikali mpya ilikuwa bila wawakilishi wa LDP tena.

Harakati ya machungwa

hariri

LDP ikaunda harakati ya ODM kama chama cha Orange Democratic Movement pamoja na KANU na kuandaa uchaguzi wa 2007. KANU ikajiondoa baadaye katika ODM lakini sehemu ya wanasiasa wake walibaki upande wa ODM.

Katika uchaguzi wa bunge wa 2007 LDP haukupeleka tena wagombea kwa jina lake ila tu kupitia ODM.