Silaha za Ufaransa zatumika katika vita vya Sudan licha ya vikwazo vya silaha vya UN - Amnesty

"Utafiti wetu unaonesha kuwa silaha zilizoundwa na kutengenezwa nchini Ufaransa zinatumika kikamilifu katika uwanja wa vita nchini Sudan," Katibu Mkuu wa Amnesty International Agnès Callamard alisema.

Muhtasari

  • Shambulio la kisu dhidi ya daktari wa India laongeza hofu ya usalama
  • Polisi Afrika Kusini watuhumiwa kuwatesa wachimbaji madini haramu
  • Sudan Silaha za Ufaransa zatumika katika vita vya Sudan licha ya vikwazo vya silaha vya UN - Amnesty
  • Brazil Mtu mmoja afariki baada ya shambulio dhidi ya Mahakama Kuu ya Brazil
  • Uganda Lugha ya Kiswahili kufundishwa Uganda kwa awamu
  • Israel na Lebanon Jeshi la Israel latangaza kuuawa kwa wanajeshi wake sita kusini mwa Lebanon
  • Sayansi Matumbawe makubwa zaidi ulimwenguni yapatikana katika Pasifiki
  • Iran Mwanaharakati ajiua akipinga utawala wa Iran
  • Paris Ufaransa yaimarisha ulinzi mechi ya Israel baada ya vurugu za Amsterdam
  • Urusi na Afrika Urusi yatuma wakufunzi wa kijeshi nchini Equatorial Guinea - ripoti

Moja kwa moja

Na Ambia Hirsi & Lizzy Masinga

  1. Tunakamilisha matangazo haya ya moja kwa moja. Hadi kesho kwaheri.

  2. Baba Rahman aahidi kurudi Black Stars atakapokuwa tayari

    xx

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Mlinzi wa Ghana, Baba Rahman, ameahidi kurudi katika timu ya taifa ya Black Stars wakati atakapokuwa na afya bora, baada ya kuuguza kwa muda mrefu majeraha.

    Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 30, ambaye anachezea PAOK nchini Ugiriki, alijitenga na majukumu ya kimataifa ili kuzingatia afya yake baada ya kuhangaishwa na majeraha aliyoyapata akichezea timu yake ikiwa ni pamoja na majeraha mawili makubwa ya goti.

    Rahman alicheza kwa mara ya mwisho kwa Ghana katika mechi ya kufuzu Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) dhidi ya Jamhuri ya Afrika ya Kati mwaka 2023, ambapo alizomewa na baadhi ya mashabiki, lakini anasema kutokuwepo kwake ni kutokana na afya yake, sio unyanyasaji aliyopata.

    Rahman, ambaye amepitia kipindi kirefu cha kupona majeraha kati ya 2017 na 2020, anazingatia kurejesha kiwango chake cha mchezo katika PAOK, ambapo amekuwa katika hali nzuri ya kucheza, akichangia magoli sita na kusaidia mabao manne msimu uliopita.

    Uchezaji wake mzuri umewavutia baadhi ya vilabu vya ligi ya uingereza , ikiwa ni pamoja na West Ham na Everton, ambao wanamfuatilia kwa karibu.

    Rahman alielezea imani yake kuhusu mustakabali wa Black Stars, licha ya changamoto zilizopo katika michuano ya kufuzu Afcon, na bado ana matumaini kuhusu nafasi ya Ghana kufuzu kwa Kombe la Dunia la 2026.

    Anajitolea kuzingatia afya yake, kupata muda zaidi wa kucheza katika klabu yake, na kurudi katika timu ya taifa wakati atakapokuwa tayari.

  3. Mtu mmoja afariki katika shambulizi la Mahakama ya Juu ya Brazil

    xx

    Chanzo cha picha, EPA

    Mwanamume mmoja ambaye alifanya jaribio la kushambulia mahakama ya juu Zaidi ya Brazil katika mji mkuu wa Brasilia jumatano jioni anaaminika kuuawa na vilipulizi alivyokuwa navyo.

    Maafisa wa polisi wamebaini kuwa anaitwa Francisco Wanderley Luiz,ambaye alibwagwa katika uchaguzi wa kansela wa aliyekuwa rais Jaie Bolsonaro’s wa chama cha Liberal.

    Aidha alipatikana amefariki nje ya jengo dakika chache baada ya milipuko miwili ambayo ilishuhudiwa katika eneo hilo.

    Waliokuwa katika eneo la mkasa wamesema kuwa waliona mwanamume huyo akirusha vilipuzi hivyo kabla ya kuvilipua,hata hivyo hakuna aliyejeruhiwa na mlipuko huo ,mafisa wasema.

    Eneo la mkasa limefungwa na sasa roboti ya kunusa bomu inatumika kutafuta mwili wa jamaa huyo.

    Polisi wanasema tayari wamepata mashine ya kutega bomu hiyo ambayo wanaamini ilikuwa ni ya vilipuzi hivyo.

    Wakili mkuu wa serikali Jorge Messias amelaani mkasa huo akiutaja ni wa makusudi na kuapa uchunguzi wa kina utafanyika.

    ‘'Ninakemea vikali mashamulizi dhidi ya mahakama ya juu zaidi na bunge ,”alisema haya kupitia ukurasa wake wa mtandao wa X.

    Mashambulizi haya yanajiri wiki moja kabla ya rais wa China Xi Jinping kuzuru taifa hilo kufuatia ziara yake ya kuelekea kongamano la G20 linaloandaliwa Rio de Janeiro.

    Mwaka jana, jengo hili lilikuwa eneo lilikuwa na vurugu baada ya wafuasi wa Bolsonaro kuvamia jengo hili baada ya rais Lula kuapishwa rasmi kuingia uongozini.

  4. Idadi ya vifo Sudan ni kubwa zaidi kuliko ilivyoripotiwa hapo awali - utafiti

    Vita nchini Sudan vimewalazimu mamilioni ya watu kutoka makwao

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Idadi ya watu wanaofariki kutokana na vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Sudan ni kubwa zaidi kuliko ilivyoripotiwa hapo awali, kulingana na utafiti mpya.

    Zaidi ya watu 61,000 wamefariki katika jimbo la Khartoum, ambako mapigano yalianza mwaka jana, kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Utafiti la London School of Hygiene and Tropical Medicine la Sudan.

    Kati ya hao, watu 26,000 walifariki kutokana na matokeo ya moja kwa moja ya ghasia, ilisema, ikibainisha kuwa sababu kuu ya vifo kote Sudan ni ugonjwa unaoweza kuzuilika na njaa.

    Watu wengi zaidi wamefariki katika maeneo mengine nchini humo, hasa katika eneo la la Darfur, ambako kumekuwa na ripoti nyingi za ukatili na mauaji ya kikabila.

    Wafanyakazi wa misaada wanasema mzozo nchini Sudan umezua mzozo mbaya zaidi wa kibinadamu duniani, huku maelfu ya watu wakikabiliwa na tishio la njaa.

    Umoja wa Mataifa na mashirika mengine ya misaada yamekuwa yakikadiria idadi ya vifo vilivyothibitishwa kuwa 20,000 .

    Kutokana na mapigano na machafuko nchini,hakuna ya utaratibu wa kunakili idadi ya watu waliouawa.

    Utafiti huo unajiri huku shirika la kutetea haki za binadamu likisema teknolojia ya kijeshi ya Ufaransa inatumiwa katika mzozo huo, kinyume na vikwazo vya Umoja wa Mataifa vya silaha.

  5. Shambulio la kisu dhidi ya daktari wa India laongeza hofu ya usalama

    Daktari wa India

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Tukio la daktari kushambulio kwa kisu katika hospitali ya Chennai kusini mwa India limeibua umpya wasiwasi kuhusu usalama wa wataalamu wa afya nchini humo.

    Polisi wanasema kuwa Balaji Jaganathan, daktari wa saratani katika hospitali ya serikali, alidungwa kisu mara kadhaa na mwanamume ambaye inasemekana hakuridhishwa na matibabu ya mamake.

    Hali ya daktari imeripotiwa kuimarika huku mshambuliaji akizuiliwakatika kituo cha polisi.

    Zaidi ya 75% ya madaktari nchini India wamekabiliwa na aina fulani ya vurugu na 68.33% ya mashambulizi kama hayo hufanywa na waliohudhuria wagonjwa, ripoti ya Chama cha Madaktari wa India (IMA) inaonyesha.

    Tukio hilo linakuja miezi kadhaa baada ya ubakaji na mauaji ya daktari tarajali akiwa kazini kusababisha maandamano nchini nzima - na mkuibua mjadala kuhusu usalama madaktari nchini India.

    Shambulio hilo lilitokea siku ya Jumatano, wakati Bw Jaganathan alipokuwa akimtibu mamake mshambuliaji, ambaye hivi majuzi aligundulika kuwa na saratani ya ovari.

  6. Polisi Afrika Kusini kuchunguzwa kwa tuhuma za kuwatesa wachimbaji madini haramu

    xx

    Tume ya Haki za Kibinadamu nchini Afrika Kusini inasema kuwa itawachunguza polisi kuhusu operesheni yake ya kuwalazimisha wachimbaji madini haramu kutoka kwenye migodi kwa kuwanyima chakula na maji.Wachimba migodi hao, wamekuwa chini ya ardhi tangu katikati ya mwezi Oktoba na wamekataa kushirikiana na mamlaka, wakihofia kukamatwa.

    Tume hiyo inasema kuna wasiwasi kwamba operesheni ya serikali inayolenga kutatiza uchimbaji madini haramu inaweza kuwa na athari kwa haki ya kuishi.

    Hii ni baada ya mamlaka kukata chakula na maji kwa maelfu ya wachimba migodi wanaojulikana kama zama zama.

    Kundi hili ambalo linajumuisha wafanyikazi wengi waliofukuzwa kazi na wahamiaji wasio na vibali wamekuwa wakikataa kutoka kwa migodi hiyokwa kuogopa kukamatwa.

    Serikali inasema msaada hautatumwa kwa wale inaowataja kuwa wahalifu licha ya ripoti ambazo hazijathibitishwa za vifo na ugonjwa kwa wachimba migodi hao.

    Polisi waliiambia BBC kwamba, kinyume na ripoti za awali, wachimbaji hao hawajanaswa chini ya migodi hiyo -- lakini waliamua kukata huduma za kuwapachakula na maji. Maafisa wanafuatilia njia mbadala za kutoka katika mgodi huo katika eneo la Stilfontein, wakisubiri wachimbaji kujitokeza.

    Wanaaminika kukaa chini ya ardhi kwa wiki kadhaa, wakitafuta mabaki ya dhahabu na almasi. Serikali imesema haitatoa msaada wowote hadi pale watakapojitokeza.

    Msemaji wa polisi, Sabata Mokgwabone, amesema hatua za kisheria zinachukuliwa dhidi ya wachimbaji hao haramu:

    “Wale wanaotoka huko chini au wanaotolewa, tunawashughulikia kulingana na jinsi sheria inavyoeleza..hii inamanisha kwamba tunawahukumu kulingana na taifa walilotoka na vilevile tukizingatia sheria za nchi zao.

    Bw Mokgwabone pia ameshutumu kampuni za uchimbaji madini kwa kutojitokeza kusaidia maafisa wa serikali.

  7. Silaha za Ufaransa zatumika katika vita vya Sudan licha ya vikwazo vya silaha vya UN - Amnesty

    Mamlaka za Ufaransa hazijajibu shutuma

    Chanzo cha picha, Amnesty International

    Teknolojia ya kijeshi ya Ufaransa inatumiwa katika vita vya kikatili vya wenyewe kwa wenyewe nchini Sudan kinyume na vikwazo vya silaha vya Umoja wa Mataifa, shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limesema.

    Inasema wanamgambo wa RSF wanatumia magari katika eneo la Darfur yanayotolewa na Umoja wa Falme za Kiarabu ambayo yana vifaa vya Ufaransa wakati wanapambana na jeshi.

    "Utafiti wetu unaonesha kuwa silaha zilizoundwa na kutengenezwa nchini Ufaransa zinatumika kikamilifu katika uwanja wa vita nchini Sudan," Katibu Mkuu wa Amnesty Agnès Callamard alisema.

    Mamlaka za Ufaransa hazijajibu shutuma hizo huku UAE hapo awali ilikana kuipatia silaha RSF.

    Mfumo wa ulinzi wa Galix, uliotengenezwa nchini Ufaransa na makampuni ya KNDS na Lacroix, unatumika kwa vikosi vya nchi kavu kusaidia kukabiliana na mashambulizi ya karibu.

    Amnesty ilisema silaha hizo zinaweza kutumika kutekeleza au kuwezesha ukiukaji mkubwa wa haki, na kuongeza kuwa serikali ya Ufaransa lazima ihakikishe makampuni "yanasimamisha mara moja usambazaji wa mfumo huu kwa UAE".

    Unaweza kusoma;

  8. Mtu mmoja afariki baada ya shambulio dhidi ya Mahakama Kuu ya Brazil

    Maafisa wa polisi

    Chanzo cha picha, EPA

    Mtu mmoja aliyejaribu kushambulia Mahakama ya Juu ya Brazil katika mji mkuu Brasilia Jumatano jioni anaaminika kuuawa na vilipuzi vyake mwenyewe.

    Alipatikana amekufa nje ya jengo muda mfupi baada ya milipuko miwili kutikisa eneo hilo.

    Mashuhuda walisema walimshuhudia mwanaume huyo akirusha kile kilichoonekana kuwa vilipuzi kabla ya kutokea mlipuko huo.

    Hakuna mtu mwingine aliyejeruhiwa katika tukio hilo, maafisa walisema.

    Eneo hilo limefungwa na roboti ya kutegua bomu, inatumika kupekua mwili wa mtu huyo.

    Polisi wanasema wametambua kipima muda ambacho kinaweza kuhusishwa na vifaa vingine.

    Mwanasheria mkuu wa nchi hiyo, Jorge Messias, alilaani kile alichosema ni shambulio la makusudi na kuahidi uchunguzi kamili kuhusu milipuko hiyo.

    Picha za mashirika ya habari zilionesha marehemu akiwa amelala katika eneo nje ya mahakama, huku maafisa wakizunguka eneo hilo.

    "Roboti ya Jeshi la Polisi inapekua mwili wa mtu aliyefanya shambulio hilo, na kipima muda kilitambuliwa, na inawezekana kinahusishwa na vilipuzi vingine," msemaji wa polisi Maj Raphael van der Broocke alisema.

    "Vilipuzi vingine tayari vimetambuliwa karibu na mwili," aliongeza.

  9. Lugha ya Kiswahili kufundishwa Uganda kwa awamu

    Wanafunzi darasani

    Chanzo cha picha, AFP

    Kituo cha Kitaifa cha Ukuzaji Mtaala (NCDC) kimetangaza kuwa lugha ya Kiswahili itaanzishwa kama somo la lazima katika shule za msingi kwa awamu kuanzia mwaka ujao.

    Bi Grace Baguma, mkurugenzi wa NCDC, alisema uzinduzi utaanza magharibi mwa Uganda, haswa katika Jiji la Fort Portal, na wilaya za Kasese na Kabarole.

    Bi Baguma alieleza kuwa ingawa Baraza la Mawaziri liliidhinisha ufundishaji wa lazima wa Kiswahili katika shule zote za msingi nchini kote mwaka wa 2022, rasilimali chache zimechelewesha kutangazwa kote nchini.

    "Tunaanza na shule za magharibi mwa Uganda kwa sababu ya uhaba wa kifedha, kwa kuwa tunategemea fedha za serikali kwa usambazaji," alisema Jumanne alipokuwa akiwahutubia walimu wa shule za msingi wanaopata mafunzo ya mtaala mpya wa Kiswahili katika Chuo cha Ualimu cha Msingi cha Canon Apollo Core.

    "Lengo letu ni kupanua ufundishaji wa Kiswahili hadi shuleni kote nchini hatimaye," Bi Baguma aliongeza. Alisema NCDC tayari imezipatia shule hizi za awali vifaa vya kujifunzia, na walimu wamepewa mafunzo ya kutosha ili kuanza kufundisha.

    Bi Baguma alisema wanafunzi waliopandishwa daraja hadi darasa la Nne watakuwa walengwa na kwamba watafanyiwa tathmini na Baraza la Kitaifa la Mitihani la Uganda (Uneb) watakapofika darasa la Saba.

    Pia alibainisha kuwa NCDC hapo awali ilitoa ratiba za masomo matatu ya Kiswahili kwa wiki, lakini uchapishaji ulisitishwa kutokana na uhaba wa fedha.

    Hata hivyo, kwa ufadhili huo mpya, ufundishaji wa Kiswahili utaanza katika muhula wa kwanza wa mwaka ujao.

  10. Jeshi la Israel latangaza kuuawa kwa wanajeshi wake sita kusini mwa Lebanon

    .

    Chanzo cha picha, AFP

    Jeshi la Israel lilitangaza siku ya Jumatano kuwa wanajeshi wake sita waliuawa katika mapigano kusini mwa Lebanon.

    Hii inaleta idadi ya wanajeshi waliouawa katika vita na Hezbollah tangu kuanza kwa mashambulizi ya ardhini kwenye ardhi ya Lebanon mnamo Septemba 30 kufikia 47.

    Jeshi lilichapisha majina ya wanajeshi watano waliouawa katika vita hivi, huku jina la mwanajeshi wa sita likiwa bado linasubiri kuidhinishwa kuchapishwa, kwa mujibu wa taarifa ya jeshi la Israel.

    Alisema mapigano hayo yalidumu kwa saa 3, kuanzia saa 10 asubuhi hadi saa 1 jioni

    Redio ya Jeshi la Israel ilifichua kuwa mapigano hayo yalijumuisha mashambulizi mawili ya kuvizia, moja ndani ya jengo hilo na jingine nje yake, kwa makombora ya kukinga vifaru.

    IDF ilitangaza kuuawa kwa wanajeshi na maafisa 107 kutoka Brigedi ya Golani tangu Oktoba 7 mwaka jana.

    Alisema uondoaji wa askari waliojeruhiwa na waliokufa ulikuwa mgumu na jeshi "linahitaji muda" kuelewa sababu ya tukio hilo.

    Alidokeza kuwa kuna imani kwamba kuna shimo ndani ya jengo ambalo liliruhusu wapiganaji wa Hezbollah kutojeruhiwa licha ya kushambuliwa kwa bomu.

  11. Matumbawe makubwa zaidi ulimwenguni yapatikana katika Pasifiki

    Matumbawe

    Chanzo cha picha, Photograph by Manu San Félix, National Geographic Pristine Seas

    Matumbawe makubwa zaidi kuwahi kurekodiwa yamegunduliwa na wanasayansi katika Bahari ya Pasifiki ya kusini-magharibi.

    Matumbawe makubwa, ambayo ni mkusanyiko wa viumbe vingi vilivyounganishwa, vidogo ambavyo kwa pamoja huunda kiumbe kimoja badala ya miamba, inaweza kuwa na zaidi ya miaka 300.

    Ni kubwa kuliko nyangumi wa bluu, timu inasema. Ilipatikana na mpiga picha wa video anayefanya kazi kwenye meli ya National Geographic inayotembelea sehemu za mbali za Pasifiki ili kuona jinsi ilivyoathiriwa na mabadiliko ya tabia nchi.

    "Nilienda kupiga mbizi mahali ambapo ramani ilisema kulikuwa na ajali ya meli kisha nikaona kitu," alisema Manu San Felix.

    Alimuita rafiki yake wa kupiga mbizi, na wakapiga mbizi chini zaidi kuukagua. Kuona matumbawe, ambayo yako katika Visiwa vya Solomon, ilikuwa kama kuona "kanisa kuu chini ya maji", alisema.

    "Ni jambo la hisia sana. Nilihisi heshima hii kubwa kwa kitu ambacho kimekaa katika sehemu moja na kuishi kwa mamia ya miaka," alisema.

    "Nilifikiri, 'Wow, hii ilikuwa hapa Napoleon alipokuwa hai'," aliongeza. Wanasayansi kwenye msafara huo walipima matumbawe kwa kutumia aina ya kipimo cha tepi chini ya maji. Ina upana wa 34m na urefu wa 5.5m.

    Matumbawe duniani yanakabiliwa na tishio kali huku bahari ikipata joto kutokana na mabadiliko ya tabia nchi.

    Matumbawe yanaweza kuungana na kuunda miamba mikubwa ambapo samaki na viumbe vingine huishi.

    Unaweza kusoma;

  12. Mwanaharakati ajiua akipinga utawala wa Iran

    Sanjari

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Mwanaharakati mashuhuri wa haki za binadamu wa Iran amejiua akipinga kile alichokiita udikteta wa kiongozi mkuu wa Iran, Ayatollah Ali Khamenei.

    Katika chapisho kwenye mtandao wa kijamii, Kianoosh Sanjari alisema atajiua ikiwa wafungwa wanne wa kisiasa hawataachiliwa ifikapo saa 19:00 saa za nyumbani (15:30 GMT) Jumatano.

    Kifo chake kilithibitishwa saa chache baadaye na wanaharakati wenzake.

    Katika chapisho kabla ya kifo chake, alisema anatamani kwamba "siku moja Wairani" "wataamka na kushinda utumwa". Sanjari alikuwa mkosoaji mkubwa wa viongozi wa Iran na mtetezi wa demokrasia.

    "Hakuna mtu anayepaswa kufungwa kwa kutoa maoni yake," alisema kabla ya kufariki.

    "Maandamano ni haki ya kila raia wa Iran." Jumatano asubuhi, alikuwa ameandika: "Ikiwa Fateme Sepehari, Nasreen Shakrami, Tomaj Salehi na Arsham Rezaei hawataachiliwa kutoka gerezani kufikia 19:00 leo ... nitakatisha maisha yangu kwa kupinga udikteta wa Khamenei na washirika wake.

    "Wote wanne walikamatwa kwa kuunga mkono na kuhusika katika wimbi la maandamano ambayo hayajawahi kushuhudiwa kufuatia kifo cha Mahsa Amini mwenye umri wa miaka 22, aliyefariki mwaka 2022 baada ya kukamatwa na polisi wa maadili wa Iran.

    Sanjari alikamatwa mara kwa mara na kufungwa kwa harakati zake za kisiasa kati ya 1999 na 2007. Aliondoka Iran mwaka wa 2007 na kupata hifadhi nchini Norway, kabla ya kujiunga na shirika la utangazaji la Sauti ya Amerika la Kiajemi huko Washington DC.

  13. Ufaransa kuimarisha ulinzi mechi ya Israel baada ya vurugu za Amsterdam

    Polisi wa Paris wanachukulia tukio hilo kama mechi hatarishi na wanalenga kumaliza matatizo yoyote

    Chanzo cha picha, FRANCK FIFE/AFP

    Maelfu ya polisi wanatumwa mjini Paris kuhakikisha usalama wa mchezo wa kimataifa wa Ufaransa na Israel siku ya Alhamisi, wiki moja baada ya ghasia mjini Amsterdam ambapo mashabiki wa Maccabi Tel Aviv walishambuliwa.

    Mkuu wa polisi wa Paris Laurent Nuñez alisema kuwa maafisa 4,000 watakuwa doria, 2,500 katika Stade de France katika vitongoji vya kaskazini mwa Paris na wengine kwenye usafiri wa umma na ndani ya mji mkuu.

    Aidha karibu walinzi wa usalama wa binafsi 1,600 watakuwa zamu katika uwanja huo, na kitengo cha polisi cha wasomi wa kupambana na ugaidi kitalinda kikosi cha Israel kinachotembelea.

    "Ni mechi yenye hatari kubwa [kwa sababu ya] muktadha wa kisiasa wa kijiografia," Bw Nuñez alisema.

    "Hatutaruhusu jaribio lolote la kuvuruga utulivu." Mechi ya Uefa Nations League inachunguzwa vikali kufuatia vurugu baada ya mechi ya Alhamisi iliyopita kati ya Ajax na Maccabi Tel Aviv nchini Uholanzi.

    Uwanja huo unaoweza kubeba mashabiki 80,000, utajaa robo pekee.

    Kufuatia ushauri wa serikali ya Israel, si zaidi ya mashabiki 100 au zaidi wa Israel wanatarajiwa kusafiri hadi Paris, ingawa mashabiki wengine wa Israel wanaweza kuhudhuria mchezo huo.

    Wanasiasa kote Ulaya walishutumu "kurejea kwa chuki" baada ya mashabiki wa Israeli kufukuzwa katika mitaa ya Amsterdam.

    Mashabiki wa Maccabi wenyewe walihusika katika uharibifu, kuharibu bendera ya Palestina, kushambulia teksi na kuimba nyimbo za kupinga Waarabu, kulingana na mamlaka ya jiji.

    Kisha walilengwa na "vikundi vidogo vya waasi ... kwa miguu, kwa pikipiki au gari", jiji lilisema katika ripoti ya kurasa 12.

    Ghasia kati ya Israel na majirani zake katika Mashariki ya Kati zinaweza kuenea hadi Ulaya. Ufaransa, Ubelgiji na Uholanzi zote zina idadi kubwa ya Waislamu wenye asili ya Afrika Kaskazini na wanaishi kando ya Wayahudi wachache sana, ambao kimsingi wanajitambulisha sana na Israel.

  14. Urusi yatuma wakufunzi wa kijeshi nchini Equatorial Guinea - ripoti

    Marais wa Guinea ya Ikweta na Urusi walikutana mwezi Septemba

    Chanzo cha picha, AFP

    Urusi imeripotiwa kutuma hadi wanajeshi 200 nchini Equatorial Guinea kulinda kiti cha urais, huku ikiendelea kupanua uwepo wake barani Afrika.

    Ripoti za vyombo vya habari zinasema kwamba Warusi wanafundisha wanajeshi waandamizi katika miji mikuu miwili ya nchi hiyo - mji mkuu Malabo na Bata.

    Ripoti za wanajeshi wa Urusi waliotumwa nchini humo kwa mara ya kwanza ziliibuka mwezi Agosti.

    Urusi, ambayo imekuwa ikitaka kupata ushawishi zaidi barani Afrika, katika miaka ya hivi karibuni imetuma maelfu ya mamluki Afrika Magharibi na Kati ili kulinda tawala za kijeshi na kuwasaidia kupambana na waasi.

    Shirika la habari la Reuters lilinukuu vyanzo vikisema kwamba Warusi kati ya 100 na 200 walikadiriwa kufika katika kipindi cha miezi miwili iliyopita. Ilisema kuwa baadhi yao wana uwezekano wa kuwa sehemu ya Corps Africa, kikosi cha kijeshi kilichojulikana hapo awali kama Wagner kabla ya kubadilishwa jina na kuwa chini ya udhibiti wa kijeshi wa Urusi.

    Siku ya Jumatano, Tutu Alicante, mwanaharakati wa haki za binadamu mwenye makao yake nchini Marekani kutoka Guinea ya Ikweta, aliliambia shirika la utangazaji la serikali ya Marekani VOA kwamba madai ya kuwepo kijeshi nchini humo yanaweza kudhoofisha maslahi ya kijiografia ya Marekani.

    Alisema kuwa Urusi "bila shaka inaimarisha misuli yake ya kijeshi na kiuchumi" kupitia uwepo wa wanajeshi nchini humo.

    Marekani katika siku za nyuma imekuwa na uwekezaji ikiwa ni pamoja na katika sekta ya nishati ya nchi lakini maslahi yamepungua.

    Baadhi ya nchi za Afrika Magharibi ambazo zimekuwa na mapinduzi katika miaka ya hivi karibuni zimejitenga na washirika wa jadi wa Magharibi kama vile Ufaransa, zikizishutumu kwa kutofanya vya kutosha kukomesha uasi wa wanajihadi, huku zikitafuta uhusiano wa karibu na Urusi.

    Unaweza kusoma;

  15. Habari za asubuhi, karibu kwenye taarifa zetu