Pata taarifa kuu

Wimbi jipya la joto nchini Morocco laua watu 21 ndani ya saa 24

Watu 21 wamefariki katika muda wa saa 24 katika mji wa Beni Mellal, katikati mwa Morocco, kutokana na wimbi jipya la joto linaloikumba nchi hiyo, katika kipindi cha mwaka wake wa sita mfululizo wa ukame, Wizara ya Afya imesema hivi punde siku ya Alhamisi.

Kusini mwa Morocco, halijoto ilifikia nyuzi joto 45.
Kusini mwa Morocco, halijoto ilifikia nyuzi joto 45. © AFP
Matangazo ya kibiashara

Mamlaka ya Hali ya Hewa (DGM) ilitangaza wimbi kali la joto kuanzia siku ya Jumatatu hadi siku ya Jumatano katika maeneo kadhaa, na halijoto ikifikia hadi 48°C, haswa katika mji wa Beni Mellal. Katika mji huu ulioko zaidi ya kilomita 200 kusini mashariki mwa Casablanca, ambapo kipimajoto bado kilionyesha karibu digrii 43 siku ya Alhamisi, watu 21 walifariki siku ya Jumatano, kulingana na Wizara ya Afya.

Vifo vingi vinahusu watu wanaougua magonjwa sugu na wazee, joto la juu limechangia kuzorota kwa hali yao ya afya na kuwasababishia kvifo, "kurugenzi ya afya ya mkoa imesema katika taarifa yake kwa vyombo vya habari.

Wizara ya Afya imetangaza hatua za kukabiliana na athari za joto, hasa kuanzisha "saa za kudumu ndani ya vituo vya afya katika mikoa iliyoathiriwa na kuongezeka kwa joto", pamoja na uhamasishaji wa wataalamu wa afya na "utoaji wa dawa na vifaa vya hospitali".

Wizara haikuweza kubainisha mara moja ikiwa hii ndiyo idadi kubwa zaidi ya walioaga dunia baada ya wimbi la joto kali nchini. Kulingana na utabiri wa hali ya hewa, hali ya joto inatarajiwa kushuka katika siku zijazo. Huko mji wa Marrakech (kusini), ambapo hali ya joto ilifikia digrii 45 siku ya Alhamisi, itapungua digrii 10 siku ya Jumapili, kulingana na DGM.

Athari za kiuchumi

Morocco ilikuwa tayari imerekodi rekodi za joto msimu huu wa baridi, na mwezi wa joto zaidi wa Januari kurekodiwa katika nchi hii ya kifalme tangu mwaka 1940 (karibu 37°C katika maeneo mengine), kulingana na DGM. Mtandao wa European Copernicus ulitabiri kwamba rekodi za kila siku zingepitwa msimu huu wa joto katika ulimwengu wa kaskazini na kwamba sayari itastahimili kipindi kirefu cha joto kali kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa.

Mabadiliko ya hali ya hewa yanasababisha matukio ya hali ya hewa ya muda mrefu, yenye nguvu na ya mara kwa mara kama vile mawimbi ya joto na mafuriko. Nchini Morocco, ongezeko la joto pia linatishia hifadhi za mabwawa. Uvukizi wa maji umefikia "mita za ujazo milioni moja na nusu kwa siku," Waziri wa Maji Nizar Baraka alisema mwishoni mwa mwezi Juni.

Ukame pia tayari una madhara katika sekta ya kilimo, muhimu kwa uchumi wa taifa kwani inaajiri theluthi moja ya watu na inawakilisha 14% ya mauzo ya nje, faida zaidi kuliko soko la ndani. Tume ya Juu ya Mipango (HCP) ilibainisha mwezi Mei kwamba "hali ya soko la ajira inaendelea kuathiriwa na ukame" na iliripoti kwamba kiwango cha ukosefu wa ajira kiliongezeka kutoka 12.9% hadi 13.7% katika robo ya kwanza ya mwaka 2024 ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka. 2023.

Ajira 159,000 katika sekta ya kilimo zilitoweka katika kipindi hiki, na kufanya jumla ya watu wasio na ajira kufikia zaidi ya milioni 1.6 nchini, ambayo ina wakazi milioni 37. Rekodi ya juu zaidi ya halijoto katika ngazi ya kitaifa ilirekodiwa mnamo mwezi wa Agosti 2023 huko Agadir (kusini) ikiwa na 50.4°C. Ulimwenguni, Jumatatu Julai 22 ilikuwa siku ya joto zaidi katika rekodi tangu rekodi zianze mnamo 1940, Copernicus ilisema siku ya Jumatano, ikivunja rekodi iliyotangazwa siku moja kabla.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.