Nenda kwa yaliyomo

Somalia ya Kiingereza

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Pitio kulingana na tarehe 23:05, 23 Agosti 2018 na Milenioscuro (majadiliano | michango) (svg version (GlobalReplace v0.6.5))
Mahali pa Somalia ya Kiingereza

Somalia ya Kiingereza' au British Somaliland ilikuwa eneo lindwa la Uingereza katika Somalia ya Kaskazini. Eneo lake lilikuwa tangu 1961 sehemu ya Jamhuri ya Somalia na tangu 1991 limekuwa Jamhuri ya Somaliland yaani nchi isiyotambuliwa na umma wa kimataifa lakini yenye tabia zote za nchi huru.

Koloni mwaka 1884/1885

Uingereza uliingia katika eneo hili baada ya Misri kuondoka mwaka 1885 baada ya kushindwa na jeshi la Mahdi huko Sudan. Uingereza uliingia kwa sababu iliona umuhimu wa kutawala pande zote mbili za Bab el Mandeb ikihofia uenezaji wa nchi nyingine za Ulaya hasa Ufaransa iliyokuwa na koloni ya kwanza ya Ubuk (Obok) katika Djibouti ya leo tangu 1862. Pamoja na hayo Waingereza walitegemea kununua nyama kwa ajili ya mji wa Aden na meli zilizopita hapo kati ya Uhindi na Ulaya.

Somaliland ilitawaliwa awali kama mkoa wa Uhindi wa Kiingereza ikawa baadaye chini ya wizara ya koloni huko London.

Upinzani wa Mohammed Abdullah Hassan

Hata kama Uingereza haukuwa na nia ya kuingilia mno katika maisha ya wenyeji ulikutana na upinzani mkali kuanzia mwaka 1899. Kiongozi wa kidini Mohammed Abdullah Hassan aliyeitwa na Waingereza "Mullah majununi". Waingereza walijibu kwa ukali katika vita ya miaka 20 iliyoua takriban theluthi moja wa wakazi wote wa eneo.

Mwishowe Uingereza iliweza kumaliza upinzani kwa teknolojia mpya ya eropleni za kijeshi zilizotumia mabomu na bunduki za mtombo kutoka angani mara ya kwanza katika Afrika.

Vita Kuu ya Pili ya Dunia na uhuru

Wakati wa Vita Kuu ya Pili ya Dunia eneo likatwaliwa na Italia katika Agosti 1940 lakini kuchukuliwa tena na Uingereza katika Machi 1941.

Uhuru ulifika 26 Juni 1960. Tar. 1 Julai kulitokea muungano na Somalia ya Kiitalia iliyopokea uhuru wake pia.

Nchi ya pekee

Baada ya kuporomoka kwa serikali ya Somalia eneo la Somalia ya Kiingereza la awali likatangaza uhuru wake Mei 1991 kama Jamhuri ya Somaliland.