Tanga (mji)
Jiji la Tanga ni mji mkuu wa Mkoa wa Tanga uliyoko ufukoni mwa Bahari ya Hindi wenye Msimbo wa Posta namba 21100.
Jiji la Tanga | |
Mahali pa mji wa Tanga katika Tanzania |
|
Majiranukta: 5°4′12″S 39°5′24″E / 5.07000°S 39.09000°E | |
Nchi | Tanzania |
---|---|
Mkoa | Tanga |
Wilaya | Tanga |
Idadi ya wakazi | |
- Wakazi kwa ujumla | 393,429 |
Tanga ina bandari kubwa kabisa katika sehemu ya kaskazini mwa Tanzania.
Njia ya reli kwenda mji wa Moshi inaanzia hapo.
Jina la mji wa Tanga linaaminiwa kutokana na lugha ya Kibondei yaani Shamba, kwa sababu wenyeji ambao walikuwa Wabondei waliishi kisiwa cha Toten lakini shughuli zao za kilimo walizifanyia eneo ambalo kwa sasa linajulikana kama mji wa Tanga. [1]
Wakati wa sensa iliyofanyika mwaka wa 2012, jiji la Tanga lilikuwa na wakazi 273,332[2] walioishi katika kata 24 za eneo lake. Mwaka 2022 walihesabiwa 393,429 [3].
Historia
haririTanga insaemekana imeanzishwa na wafanyabiashara Waajemi katika karne ya 14 BK. Mji wa Tanga haukupata umuhimu kama mji wa jirani wa Mombasa. Tarihi ya Pate inasema ya kwamba kabla ya kuja kwa Wareno Pate iliwahi kutawala Lindi kwa muda fulani.
Katika karne ya 19 Tanga ilikuwa chini ya utawala wa Omani na Zanzibar. Misafara ya biashara ilianzia hapo kwenda bara. Tangu Zanzibar kuwa mji mkuu wa Sultani wa Omani sehemu ya misafara ilihamishwa kwenda Bagamoyo na Pangani yaani bandari zilizokuwa karibu zaidi na Unguja, hivyo umuhimu wa Tanga ulipungua.
Baada ya kuanzishwa kwa ukoloni wa Kijerumani (DOA) mji ulikuwa makao makuu ya mkoa wa Tanga. Sasa bandari ya Tanga iliongezeka umuhimu kwa sababu -tofauti na bandari nyingi za miji ya Waswahili- meli kubwa ziliweza kuingia ndani ya bandari na kukaa salama. Wajerumani walijenga vifaa vya bandari ya kisasa pamoja na reli kutoka Tanga kwenda Moshi. Reli iliwezesha kilimo kwa ajili ya soko la dunia Tanga ikawa bandari kuu kwa ajili ya katani na kahawa. Hivyo mji ulikua haraka.
Wakati wa Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia Tanga iliona mapigano makali tarehe 3 - 5 Novemba 1914. Jaribio la Uingereza kuvamia Tanga kwa kikosi cha askari 8000 Waingereza na Wahindi kutoka meli kwenye Bahari Hindi ilishindwa vibaya na Jeshi la Ulinzi wa Kijerumani chini ya uongozi wa Paul von Lettow-Vorbeck.
Baada ya Uingereza kuchukua utawala wa Afrika ya Mashariki ya Kijerumani reli ya Tanga-Moshi iliunganishwa na Reli ya Kati, hivyo ikawa na njia kwenda Dar es Salaam pia.
Mwaka 1922 "Tanganyika Territory African Civil Services Association" (TAA) iliundwa Tanga ambayo ilikuwa shirika ya kwanza ya Kiafrika yenye shabaha za kisiasa.
Kutokana na kupanuka kwa bandari ya Dar es Salaam umuhimu wa bandari ya Tanga umerudi tena nyuma.
Tanga katika tamaduni maarufu
haririTanga ni mji ambao sifa zake zilianza kusikika kuanzia enzi za utawala wa Wajerumani, jiji ambapo shule ya kwanza ya serikali ilijengwa enzi hizohizo za utawala wa Wajerumani, jiji ambalo liliendelea kukua sana kutokana na kilimo cha katani na hivyo kukusanya vijana toka kila kona ya nchi kuja kutafuta kazi katika mashamba makubwa ya katani wakati huo.
Tanga ni mji ambao kutokana na wingi wa vijana wakati huo, shughuli za burudani ya muziki nazo zilifikia kiwango cha juu kuliko sehemu nyingi Tanzania.
Ukizungumzia historia ya muziki wa dansi, huwezi kukwepa kuzungumzia Tanga, kwani historia inatueleza kuwa kabla ya kuanza vikundi vya muziki wa dansi kulianzishwa klabu za kucheza dansi. Klabu hizo zikitumia muziki wa santuri, wanachama wake walicheza na hata kushindana kucheza muziki kwa mitindo mbalimbali ya kigeni ikiwemo waltz, tango, chacha, rumba na kadhalika.
Klabu za kwanza nchini zilianzia Tanga. Kulikuwa na klabu kama Young Noverty miaka michache baada ya Vita ya Kwanza ya Dunia, wakati huo nchi ya Tanganyika ikiwa bado changa kabisa. Mtindo huu wa vilabu vya dansi ulienea na baadaye kuingia Dar es Salaam na miji mingine iliyokuwa imeshaanza wakati huo. Vilabu hivi ndivyo baadaye vilivyanzisha vikundi vya kwanza vya muziki wa dansi. Hata majina ya vikundi hivyo vya kwanza yalihusiana na klabu za burudani za wakati huo. Kulikuwa na vikundi kama Coast Social Orchestra, Dar es Salaam Social Orchestra na kadhalika.
Hivyo mji wa Tanga ulikuwa katika ndoto za vijana enzi hizo. Kwa vile vijana wengi walikusanyika katika jiji hilo, kulianzishwa pia klabu ambazo zilikuwa kwa ajili ya vijana waliokuwa wakitoka kabila moja. Klabu hizo zikiwa na nia ya wanachama wao kusaidiana katika shida na raha, na vilabu hivyo pia vilikuwa sehemu muhimu katika kutoa burudani kwa vijana waliotoka sehemu moja.
Kati ya klabu hizo kulikuweko na klabu iliyoitwa Young Nyamwezi: kama jina lake lilivyo ilikuwa klabu ya vijana kutoka Unyamwezi. Hatimaye mwaka 1955 klabu hiyo ilianzisha bendi yake iliyoitwa Young Nyamwezi Band, bendi hiyo ilikuja kukua na baada ya uhuru ilibadili jina na kuitwa Jamhuri Jazz Band. Hakika kwa vijana waliokuwa wapenzi wa muziki miaka ya 1960 na 1970 ilikuwa lazima uifahamu Jamhuri Jazz Band, muziki wake, au kwa lugha ya enzi zile, ‘vibao’ vyake vilivyojulikana Afrika ya Mashariki nzima. Bendi hiyo ilikuwa ikibadili mitindo ya upigaji wake na kupiga katika mitindo ya ‘Toyota’ na hatimaye ‘Dondola’. Aliyekuja kumiliki bendi hiyo, ambayo wapenzi wake pia waliita JJB alikuwa Joseph Bagabuje, kulikuwa hata maelezo wakati fulani kuwa JJB ilikuwa kifupi cha Joseph Jazz Band na si Jamhuri Jazz Band. Kama ilivyokuwa kawaida ya bendi za wakati ule Jamhuri Jazz Band ilisafiri sana na kufanya maonyesho katika kila kona ya nchi, jambo hilo pamoja na kuwa bendi hii ilirekodi na kutoa santuri kupitia kampuni za kurekodi za Kenya na pia kurekodi nyimbo zake katika radio ya Taifa uliifanya bendi hiyo kuwa maarufu sana.
Upigaji wa aina ya pekee wa gitaa la rhythm wa bendi hii, ambao uligunduliwa na Harrison Siwale, maarufu kwa jina la Sachmo, uliigwa na wapiga gitaa ya rhythm wengi nchini. Uimbaji wa kutumia waimbaji wawili tu, uliopendelewa na bendi za Tanga wakati huo ikiwemo bendi nyingine maarufu ya Atomic jazz Band, ulikuwa wa aina yake pia.
Jamhuri Jazz Band pia ndiyo ilikuwa chanzo cha bendi maarufu ya Simba wa Nyika. Inasemekana kuwa siku ambayo Jamhuri Jazz Band ilikuwa imekodishwa kwa ajili ya kupiga kwenye harusi kule Muheza. Wanamuziki walikuwa wakilazimika kukusanyika katika jengo la klabu lililokuwa Barabara ya 15 ili kupata usafiri wa kwenda Muheza. Siku hiyo wanamuziki wengine walikusanyika lakini George na Wilson Peter, Luza Elian na wengine wachache hawakuonekana. Baada ya upelelezi mfupi ikajulikana kuwa wamejificha au wameondoka mjini Tanga, hivyo ikalazimika kutafuta wanamuziki viraka wa harakaharaka kuweza kufanikisha onyesho la siku hiyo. Hivyo mtu ambaye hakuwa mwanamuziki bali shabiki tu wa bendi aliweza kupanda jukwaani na kuimba katika harusi hiyo. Hali haikuwa mbaya kwani alijitokeza mteja mwingine akitaka bendi ikapige kwenye harusi yake pia, lakini ombi lake lilikataliwa kwani wanamuziki walijua kuwa hawakuwa kwenye kiwango chao. Baada ya hapo kikaanza kipindi kigumu kwa Jamhuri Jazz Band kujitahidi kurudisha hadhi na ubora wa bendi, na pia ikaanza safari iliyokuja kubadili historia ya muziki wa dansi Afrika mashariki kwa vijana hao waliotoroka kuelekea Arusha ambako walianzisha Arusha Jazz Band na hatimaye kuvuka mpaka na kuingia Kenya ambako walianzisha Simba wa Nyika ambayo mafanikio yake yanatingisha hisia za wapenzi wa muziki wa dansi mpaka leo.
Hata hivyo Tanga haikubaki nyuma kwenye Muziki wa Taarab[4]
Vivutio vya utalii vya Tanga
haririTazama pia
haririMarejeo
hariri- ↑ linganisha makala "Tanga" katika Kamusi ya Koloni za Kijerumani
- ↑ "Sensa ya 2012, Tanga - Tanga CC" (PDF). Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo (PDF) mnamo 2016-03-03. Iliwekwa mnamo 2016-05-16.
- ↑ https://www.nbs.go.tz
- ↑ "Habari za Tamaduni maarufu jijini Tanga katika blogu ya Anko J Kitime". Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo 2017-01-10. Iliwekwa mnamo 2016-10-13.
Viungo vya Nje
haririKata za Wilaya ya Tanga - Tanzania | ||
---|---|---|
Central • Chongoleani • Chumbageni • Duga • Kiomoni • Kirare • Mabawa • Mabokweni • Magaoni • Majengo • Makorora • Marungu • Masiwani • Maweni • Mnyanjani • Msambweni • Mwanzange • Mzingani • Mzizima • Ngamiani Kaskazini • Ngamiani Kati • Ngamiani Kusini • Nguvumali • Pongwe • Tangasisi • Tongoni • Usagara |
Makala hii kuhusu maeneo ya Mkoa wa Tanga bado ni mbegu. Je unajua kitu kuhusu Tanga (mji) kama historia yake, biashara, taasisi zilizopo, watu au utamaduni? Labda unaona habari katika wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. Tafadhali usiingize majina ya maafisa au viongozi wa sasa maana wanabadilika mno. |