Hussein Ramadhani Mkiety (20 Machi 1987 - 26 Novemba, 2012) alikuwa msanii wa maigizo na mwimbaji na mchekeshaji wa filamu kutoka nchini Tanzania. Anajulikana sana kwa uhusika wake Sharo Milionea, jina ambalo linatokana na Sharobaro. Ili kujitofautisha na Sharobaro ambaye hali halisi ni Bob Junior na studio yake, yeye akaamua kujiita Sharo Milionea - ambapo kiasili alilitoa katika filamu aliyoigiza. [1]

Hussein Mkiety
Amezaliwa Hussein Ramadhani Mkiety
(1987-03-20)Machi 20, 1987 Lusanga, Muheza, Tanzania
Amekufa Novemba 26, 2012 (umri 25) Tanga, Tanzania
Kazi yake Mwigizaji, mtunzi, mwimbaji
Miaka ya kazi 2006 - 2012

Mkiety ni moja kati ya wasanii waliobukia Kiwalani kama vile P. the MC, Dknob, Shukuru Kilala, Darassa, Snura Mushi Jay Maswagger na wengine kibao. Alianza harakati za kwa kujihusisha shughuli za hapa na pale, kabla ya kukutana na mwongozaji maarufu wa Kiwalani Siasa Mohammed almaarufu (Chiba). Filamu yake kwanza kucheza ilikuwa Zinduna kisha Itunyama aliyoshiriki pamoja na Adrian Siaga, Shukuru Kilala na Snura Mushi. Filamu hiyo iliongozwa na Gumbo Kihorota.

Miongoni mwa filamu alicheza ni pamoja na Swagger, Oh Mama, Sharo Milionea, Jazba, Porojo, Askari wa Bushi, Machimbo. Kwa upande wa usanii wa muziki, alianza na jina la Seni Star na Zero kabla kuhamia katika jina la Sharo Milionea. Baadhi ya nyimbo alizoimba ni pamoja na Chuki Bure alioshirikiana na Dully Sykes wakati huo akiwa chini ya Ostaz Juma na Musoma. Wimbo huo ulitengenezwa na C9 wa Kiri Records mwaka 2012 na kutoka mwaka huohuo. Vilevile alipata kushiriki kwenye mfululizo maarufu wa TV Siri ya Mtungi. Sehemu ya 12 ya Siri ya Mtungi ilitolewa kama kumbukumbu kwake kwa ushirika alioufanya katika tamthilia hiyo.[2]

Kazi na maisha

hariri

Maisha ya awali

hariri

Mkiety ni mtoto wa mwisho wa familia ya watoto watatu wa Ramadhani na Zainabu Mkieti. Alizaliwa tarehe 27 Oktoba, 1985 katika kijiji cha Lusanga, Muheza, Tanga.Alipata elimu ya msingi katika shule ya Lusanga na baadaye kujiunga na sekondari ya Kwabutu alikosoma hadi kidato ya tatu, akaacha shule kutokana na matatizo ya kifamilia. Mwaka 2003 baada ya kuona maisha hayaendi, aliamua kuhamia Kiwalani, Dar es Salaam, kuungana na mama yake ambaye alikuwa mjasiriamali mdogo.Baada ya kufika Dar, alipelekwa kujifunza masuala ya ufundi magari kwenye gereji moja ambako alidumu wiki mbili na baadaye kupelekwa kwenye ufundi mafriji ambako alijifunza kwa wiki tatu, nako hakudumu baada ya kuona kipato hafifu. Kuanzia hapo akaamua kuhamia kwenye biashara ndogo na hasa ilikuwa kuuza magazeti hukohuko Kiwalani.[3]

Mwaka wa 2005, akiwa na marafiki wengine kutoka Kiwalani, ikiwa ni pamoja na Snura Mushi, Nas na Dax waliunda kundi lao la muziki na kuandaa nyimbo kadhaa, lakini kundi hilo halikudumu baada ya Snura kujiengua na kwenda kuigiza mfululizo wa filamu ya TV ya Jumba la Dhahabu. Yeye akajiunga na kundi la maigizo la Jamal Arts lililokuwa chini ya Gumbo Kihorota. Huku alikutana na Shukuru Kilala, Furaha Kiyato, Snura na watoto wengi wa Kiwalani na Yombo Vituka. Kwa Gumbo, alipata kucheza katika Zinduna na Itunyama ambazo zote zilikuwa za kiasili. Vilevile akiwa huku alikutana na wasnaii wengi ambao baadaye walikuja kuwa maarufu zaidi ikiwa ni pamoja na Emmanuel Mgaya (Masanja), Alex Chalamila (McReagan).

Sharoa vilevile aliwahi kutunga filamu moja iliyoitwa "Dakika Moja" kabla ya kubadilishwa jina na Snura na kuiita "Sekunde Chache". Kwa upande wa filamu za vichekesho, alicheza kwa mara ya kwanza katika filamu "Mbwembe Vol 2" ambayo alicheza kama "Brazamen". Baadaye katika "Vichwa Vitatu" kabla ya kuliamsha dude mazima katika Sharobaro na Sharo Milionea. Kazi hizi zilipelekea kupatwa kusaini mkataba na Khalfan Abdallah anayemiliki kundi la Bongo Super Stars Comedy ambalo linawashirikisha waigizaji kadhaa akiwamo King Majuto na Masele.

Sharo ndiye msanii wa kwanza wa vichekesho nchini Tanzania kufanya ucheshi bila kuvaa midabwada. Awali ilionekana kawaida sana kwa mchekeshaji kuvaa midabwada ili aonekane anachekesha. Au kuvaa nguo zenye mwonekano wa kipekee tofauti na hali ya kawaida. Hili alionesha mapinduzi ya hali ya juu. Baadaye alikuja kushiriki katika filamu ya Chumo iliyoongozwa na Jordan River yenye maudhui ya kupambana na ugonjwa wa malaria. Vilevile amepata kuonekana katika video ya "Sababu ya Ulofa" ya Top C. Alifamika sana kwa staili yake ya "Ooh mama" ambayo ndiyo ilikuja kuwa kama alama ya kumtambulisha Sharo katika kila kazi. Vilevile alikuwa na uhusiano wa karibu na King Majuto, ambaye walishiriki ote katika filamu ya Alosto.

Mnamo tarehe 26 Novemba, 2012 ni siku ambayo alipata ajali hukohuko Tanga akiwa sio mbali sana na nyumbani kwa mama yake ambako alikuwa anaenda kusamlimu. Ajali ilitokea saa mbili usiku, huku ikitipotiwa kuwa mwendokasi ndiyo kiini cha ajali hiyo. Hussein alikuwa anaenda Tanga kwa mama yake kumpatia fedha kwa ajili kulimia shamba na baadaye aanze ujenzi wa nyumba imara kwa ajili ya mama yake mzazi. Alikuwa anaendesha gari aina ya Toyota Harrier.[4][5] Kifo kiligubikwa na dhana nyingi za ushirikina, huku marafiki wa karibu (Kitale) wakiweweseka juu ya kuondoka mapema duniani kwa Sharo.[6]

Baadhi ya filamu zilizochaguliwa

hariri

Marejeo

hariri
  1. Mkity katika Archived 4 Julai 2017 at the Wayback Machine. Bongo Cinema.com
  2. Sehemu ya 12 ya Siri ya Mtungi.
  3. Anastazia Anyimike na mahojiano yake na Sharo - Habari Leo
  4. Ajali iliyotikisha Sharo Gazeti la Mwananchi - Ajali ilivyokatisha maisha ya Sharo Milionea
  5. Familia ya Sharo yaibua mazito Gazeti la Mwananchi la 6 Disemba, 2012.
  6. Kitale, Sharo bado hajaondoa machoni mwangu Millard Ayo - 2014.
  Makala hii kuhusu mwigizaji filamu fulani bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Hussein Mkiety kama wasifu wake, habari za maisha au kazi yake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.