Ambohimanga
Ambohimanga ni jina la mlima karibu na Antananarivo katika Madagaska. Katika karne ya 18 ilikuwa makao makuu ya sehemu ya wafalme wa Wamerina walioteka kutoka hapa sehemu nyingine za Imerina ikaendelea kuwa mahali pa makaburi ya wafalme wa Madagaska hadi mwaka 1897. Tangu mwaka 2001 imeandikishwa katika orodha ya urithi wa dunia ya UNESCO.
Jina
haririAsili ya jina Ambohimanga ni maneno mawili ya Kimalagasi: ambohi inayomaanisha "kilima" na manga inayomaanisha "takatifu" [1]. Jina lilitolewa na mfalme Andriamasinavalona wakati wa karne ya 18[2]
Maana ya kihistoria na ya kiroho katika Madagaska
haririMlima huu pamoja na "rova" (boma la wafalme) juu yake hutazamwa kama ishara muhimu zaidi wa utamaduni wa Wamerina. Pia ni kumbukumbu bora iliyohifadhiwa ya Ufalme wa Madagaska ya enzi kabla ya ukoloni na ufalme wa Imerina. Kuna ikulu na makaburi ya wafalme mbalimbali yenye maana ya kiroho kwa Wamadagaska wengi.
Hadi leo miiko mbalimbali huheshimiwa na wakazi wa vijiji walio karibu na mlima kama vile kuepukana na mahindi, mboga, nguruwe, vitunguu, matumizi ya nyasi katika upishi na kukata kuni kwenye msitu mtakatifu mguuni pa mlima [3].
Ambohimanga ilikuwa mahali muhimu tangu mwanzo wa karne ya 18 wakati mfalme Andriamasinavalona (1675–1710) aligawa Imerina kwa robo nne na kumpa mwanawe Andriantsimitoviaminiandriana robo ya kaskazini magharibi. Ugawaji huo ulisababisha vita vya wenyewe kwa wenyewe vya miaka 77. Watawala wa Ambohimanga walioboresha kuta za mji wao na kuenea. Mfalme Andrianampoinimerina aliweza kuunganisha Imerina chini ya utawala wake hadi mwaka 1793. Baadaye alirudisha ikulu yake katika mji mkuu wa kihistoria Antananarivo akitangaza miji yote miwili kuwa mji mkuu na Ambohimanga kuwa mji mkuu wa kiroho. Yeye mwenyewe na wafalme waliomfuata walifika huko kwa ibada za kifalme na kupata makaburi yao hadi Ufaransa ilivamia Madagaska na kuhamisha familia ya kifalme nje ya kisiwa.
Msitu mtakatifu
haririSehemu ya chini ya mlima inafunikwa na msitu ambao ni mabaki ya misitu asilia iliyojaa nyanda za juu za Madagaska. Miti mbalimbali huwa na maana ya kiroho ikitumiwa kwa ibada ya mizimu.
Majengo ya ngome
haririSehemu ya juu ya mlima penye ikulu na makazi zimezungukwa na mifereji ya ulinzi yenye urefu hadi mita 30 na kuta imara. Kuna mageti imara 14 yaliyofungwa kwa duara ya jiwe [4]. Kila geti lina jina la pekee na geti moja ilikuwa haki ya mfalme pekee kulipitia. Katika karne ya 19 wageni wa nje walikataliwa kuingia geti lolote.
Ikulu za kifalme
haririKuna majengo ya ikulu 3 zilizohifadhiwa mlimani.
Kufuatana na mapokeo ya Wamerina majengo wa watu hai yalijengwa kwa ubao na zana zilizotokana na mimea (zana hai), lakini majengo kwa wafu kama makaburi yalitengenezwa kwa kutumia mawe. Mwishoni mwa karne ya 19, baada ya kutokea kwa moto, matumizi ya jiwe yaliruhusiwa pia kwa majengo ya makazi. Tangu mwaka 1966 majengo mengi yaliona matengenezo kulingana na desturi za kale.
Kuna sehemu 3 za ikulu zenye majengo na makazi ya wafalme mbalimbali ambayo ni ikulu za Bevato, Mahandrihono na Nanjakana.
Sehemu ya majengo, hasa ya Bevato, yalibomolewa na wakoloni Wafaransa waliotaka kuondoa maana ya kiroho katika mahali, wakilenga kudhoofisha kumbukumbu ya utamaduni wa kale. Waliteneneza majengo mengine na mengine kati ya haya majengo ya kikoloni yalibomolewa tena baada ya uhuru.
Makaburi ya Kifalme
haririKiasili kulikuwa na makaburi 12 ya kifalme [5]. Wafaransa walihamisha makaburi ya wafalme kwenda Atananarivo mwaka 1897 na zawadi za mazishi kuonyeshwa kwenye makumbusho ya ethnolojia ya Antananarivo. Walikuwa na shabaha ya kuvunja roho ya upinzani kati ya wazalendo.
Serikali ya Madagaska iliamua mwaka 2008 kutengeneza makaburi upya na kurudisha mifupa ya wengine hapo.
Tazama pia
haririMarejeo
hariri- ↑ jean Claude Hernert, "Manga", katika Allibert, Claude; Rajaonarimanana, Narivelo (2000). L'extraordinaire et le quotidien: variations anthropologiques (Kifaransa). Paris: Karthala Editions. ISBN 978-2-84586-083-4., uk. pp. 388, 406–407.
- ↑ Labourdette, Jean-Paul; Auzias, Dominique (2011). Madagascar (Kifaransa)], Paris: Petit Futé. ISBN 978-2-7469-4029-1. Kurasa 187–188
- ↑ Raharijaona, Dr.; Raharijaona, Mme. (1931). "Anciennes residences royales: Essai de monographics sur Ambohimanga et Ambositra" (Kifaransa. Bulletin de l'Académie malgache (in French) 14: 111–136. ilitazamiwa aprili 2016
- ↑ Royal Hill of Ambohimanga (Unesco)
- ↑ Nativel, Didier (2005). Maisons royales, demeures des grands à Madagascar (Kifaransa). Paris: Karthala Editions. ISBN 978-2-84586-539-6.